Kwa lengo la kuimarisha uelewa wa umma kuhusu masuala ya sheria, demokrasia na uchaguzi, Chama cha Mawakili wa Serikali (SALA) kimeandaa kongamano la kitaifa la sheria litakalofanyika Juni 21, 2025, jijini Dar es Salaam, ambapo Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne, Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, anatarajiwa kuwa mgeni rasmi.
Kongamano hilo litakalobeba kaulimbiu “Demokrasia kwa vitendo: Sheria, Wajibikaji na Uchaguzi Mkuu 2025”, linalenga kuwajengea wananchi uwezo wa kuelewa sheria zinazoongoza chaguzi pamoja na kuwahamasisha kushiriki katika utunzaji wa amani na mshikamano wa kitaifa kuelekea uchaguzi mkuu.
Akizungumza na waandishi wa habari, Rais wa SALA, Bw. Bavoo Junus, amesema kongamano hilo ni jukwaa mahsusi la kuelimisha jamii kuhusu sheria za uchaguzi, wajibu wa kila mwananchi, na namna ya kuepusha migogoro inayoweza kutokea katika kipindi hicho nyeti.
“Tunataka wananchi wazifahamu sheria za uchaguzi kwa kina. Tutazichambua sheria hizo moja baada ya nyingine ili kuwajengea uwezo wa kushiriki kikamilifu katika uchaguzi kwa kufuata taratibu,” amesema Bw. Junus.
Aidha, amesema kongamano hilo litajadili pia njia bora za utatuzi wa migogoro ya uchaguzi na kuhimiza umuhimu wa kulinda amani, kwa kuzingatia kuwa maisha yanaendelea hata baada ya uchaguzi.
“Ni muhimu wananchi, wanasiasa na wadau wote watambue kuwa tofauti za kisiasa hazipaswi kuwa chanzo cha mgawanyiko. Lazima tukumbuke kuwa yale yanayotufanya kuwa wamoja ni mengi kuliko yanayotutenganisha,” amesema.
Bw. Junus amesisitiza kuwa kongamano hilo ni wazi kwa watu wote bila malipo, likiwahusisha wananchi wa kawaida, wanasheria, wanataaluma na viongozi kutoka ndani na nje ya nchi.