OR – TAMISEMI
Afisa Ustawi wa Jamii Ofisi ya Rais TAMISEMI Bi. Amina Mfaki, amesema Ofisi ya Rais TAMISEMI kupitia Idara ya Afya, Lishe na Ustawi wa Jamii imekuwa ikifanya jitihada mbalimbali katika kuhudumia watoto wanaoishi na kufanya biashara katika Mazingira Hatarishi (MVC) kwenye Mamlaka za Serikali za Mitaa kwa kushirikishana na Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum.
Bi. Mfaki ametoa wasilisho hilo tarehe 17 Juni, 2025 katika semina ya kuwajengea uwezo baaadhi ya Wakurugenzi kutoka kwenye Halmashauri zenye ongezeko kubwa la Watoto wa Mitaani na zinazokuwa kwa kasi waliokutana Jijini Mwanza katika ukumbi wa Gold Great kwa lengo la kujifunza namna bora ya uanzishwaji wa Madawati ya Ustawi wa Jamii katika stendi za mabasi.
Amesema Ofisi ya Rais TAMISEMI imekuwa ikisimamia uanzishwaji wa vituo jumuishi vya malezi katika Halmashauri ambavyo vimekuwa vikisaidia watoto hao.
Pia, amesisitiza kuwa, kuna umuhimu wa kutenga bajeti kwa ajili ya huduma za watoto walioko katika Mazingira Hatarishi ngazi ya Halmashauri, ikijumuisha uendeshwaji wa Dawati la Huduma za Ustawi wa Jamii katika stendi za Mabasi.
Naye, Afisa Ustawi wa Jamii Mkoa wa Mwanza Bw. Baraka Makona, amesema Mkoa huo umeamua kuandaa Mkakati Maalum wa kupambana na changamoto za ongezeko la watoto wanaoishi na kufanya biashara mitaani lengo likiwa ni kuimarisha mifumo ya kuzuia watoto kuondoka katika familia na kwenda kuishi mitaani pamoja na kuongeza uelewa wa jamii kuhusu umuhimu wa malezi, matunzo na ulinzi wa watoto kwa ujumla.