Na Silivia Amandius.
Bukoba.
Wakulima wa zao la kahawa mkoani Kagera wametakiwa kuzingatia udhibiti wa ubora wa kahawa kuanzia hatua ya uvunaji hadi usindikaji, ili kuongeza thamani ya zao hilo na kujiongezea kipato. Wito huo umetolewa na Ndugu Steven Mtambuzi, Mdhibiti Ubora kutoka Chama Kikuu cha Ushirika cha TANICA, wakati wa mafunzo maalum yaliyoandaliwa na shirika la Café Africa Tanzania kwa ajili ya wakulima wa kahawa katika mkoa huo.
Akizungumza katika mafunzo hayo, Mtambuzi alisema wakulima wengi wamekuwa wakikosa mapato kutokana na ukosefu wa elimu ya usimamizi bora wa ubora wa kahawa, jambo linalochangia kuwachelewesha katika maendeleo ya kiuchumi. Alisisitiza kuwa kwa kuzingatia viwango vya ubora, wakulima wana nafasi kubwa ya kupata masoko ya uhakika na bei nzuri zaidi ya kahawa yao.
Kwa upande wake, Afisa Kilimo kutoka shirika la Café Africa Tanzania, Bi Prisca Mtema, alisema lengo la mafunzo hayo ni kuwawezesha wakulima kupata uelewa mpana wa namna ya kutunza ubora wa kahawa kuanzia shambani hadi inapoingia sokoni. Alibainisha kuwa elimu hiyo itasaidia wakulima kuongeza tija, kuepuka hasara zisizo za lazima, na kuchangia katika ukuaji wa uchumi wa kaya zao.
Baadhi ya wakulima walioshiriki katika mafunzo hayo, akiwemo Bi Regina Kokwenda na Ndugu Joseph Kyamuangile kutoka katika vyama vya ushirika vya Missenyi na Bukoba Manispaa, wameeleza kufurahishwa na mafunzo hayo wakisema yamekuwa chachu ya mabadiliko chanya. Wameahidi kwenda kutumia ujuzi walioupata kuboresha uzalishaji na usindikaji wa kahawa, huku wakilipongeza shirika la Café Africa Tanzania kwa mchango wake mkubwa katika kuwawezesha wakulima kupitia elimu yenye tija.
Kwa ujumla, mafunzo hayo yameonekana kuwa na umuhimu mkubwa katika kuinua ubora na thamani ya kahawa ya Kagera, ambayo ni miongoni mwa kahawa bora kabisa duniani.