Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) limepata mafanikio makubwa ya kifedha katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, likiongeza mapato yake kutoka shilingi bilioni 125 mwaka 2019 hadi kufikia shilingi bilioni 189 mwaka 2024 — ongezeko la asilimia 33.1.
Akizungumza na wahariri jijini Dar es Salaam jana, baada ya kufanya ziara ya ukaguzi katika miradi mitatu, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika hilo, Bw. Hamadi Abdallah Hamad alisema ukuaji huo unadhihirisha uimarishaji wa nafasi ya shirika hilo katika sekta ya ujenzi wa nyumba nchini.
Aliitaja miradi iliyotembelewa kuwa ni Mradi wa Makazi wa Samia housing scheme (SHS), Mradi wa 711 na Golden Premier Resident (GPR).
Alisema mafanikio hayo yanatokana na uwekezaji wa kimkakati, usimamizi thabiti wa mali pamoja na azma ya dhati ya kupanua upatikanaji wa makazi nafuu kwa Watanzania.
Bw. Hamad alieleza kuwa matokeo ya ongezeko hilo la mapato yamechangia kuongezeka kwa gawio linalolipwa serikalini kutoka shilingi milioni 550 mwaka 2019 hadi kufikia shilingi bilioni 5.5 mwaka huu.
Katika mwaka wa fedha uliomalizika (Julai 2023 hadi Juni 2024), shirika limekusanya shilingi bilioni 36.8 kutokana na upangishaji wa nyumba — sawa na asilimia 112.5 ya lengo lake, hivyo kuvuka matarajio.
“Lengo letu kwa mwaka ujao wa fedha ni kukusanya takribani shilingi bilioni 10 ili kuendelea kutekeleza malengo yetu,” alisisitiza.
Aidha, Mkurugenzi huyo alifafanua kuwa thamani ya mali za NHC imepanda kutoka shilingi trilioni 5.08 hadi trilioni 5.6, na matarajio ni kuongezeka zaidi katika mwaka wa fedha ujao.
Alisema shirika liko katika hatua ya kuangalia uwezekano wa kuingia rasmi katika soko la Hisa kwa ajili ya kupata fedha za kutekeleza miradi mikubwa.
Katika hatua nyingine, Bw. Hamad alitangaza mpango huo wa miaka Saba utatekelezwa kupitia Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE) kwa lengo la kukusanya fedha za kukamilisha miradi mikakati nchini.
Dhamana hiyo itakayopewa jina la “Nyumba Bond” inalenga kuhakikisha kuwa miradi ya Makazi ya Samia inakamilika ifikapo mwaka 2030.
“Kipaumbele chetu ni kuhakikisha kuwa miradi hii, hususan ya Samia Housing Scheme, inakamilika kwa wakati kama sehemu ya mchango wetu katika kutoa makazi bora kwa wananchi,” alisema.
Alihitimisha kwa kusema kuwa mikakati ya baadaye ya NHC ni pamoja na kununua ardhi kwa bei nafuu ili kuwezesha ujenzi wa makazi ya gharama nafuu, hasa kwa Watanzania wa kipato cha chini na cha kati.