Mkurugenzi mkuu wa mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA), Bw. Adam Fimbo akizungumza na wadau mbalimbali na waandishi wa habari katika kikao kazi cha wadau wa habari katika kikao kazi cha wadau wa habari.
Wanahabari wakiwa picha ya pamoja na viongozi mbalimbali wa Mamlaka ya Cahkula na Dawa (TFDA) katika kikao kazi cha wadau wa habari.
*************************************
NA EMMANUEL MBATILO
Kwa mujibu wa takwimu za Shirika la Afya Duniani (WHO) takribani watu milioni 600 duniani sawa na mtu mmoja kati ya watu 10 huugua kutokana na kula chakula kisicho salama na kati yao, 420,00 hufariki na kati ya wanaofariki 125,000 ni watoto wenye umri wa chini ya miaka mitano.
Ameyasema hayo leo Mkurugenzi mkuu wa Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA), Bw. Adam Fimbo katika kikao kazi kwa ajili ya kuwaongezea uwezo wahariri na waandishi wa habari katika kuelimisha jamii juu ya masuala ya usalama wa chakula.
Akizungumza na wanahabari wilayani Bagamoyo mkoa wa Pwani, mkurugenzi huyo amesema kuwa pamoja na athari za kiafya ni vema kufahamu pia kuwa magonjwa yatokanayo na chakula huzorotesha shughuli mbalimbali za uzalishaji wa mali, huongeza gharama za matibabu, hudhoofisha hali ya uchumi katika ngazi zote na kusababisha athari za kijamii.
“Tatizo hili ni kubwa zaidi barani Afrika, ambapo Zaidi ya watu milioni 91 wanakadiriwa kuugua na watu 137,000 hufariki kila mwaka kutokana na kula chakula kisicho salama hivyo kubainisha kuwepo tatizo kubwa la uchafuzi wa chakula kutokana na kutozingatia kikamilifu kanuni bora za usafi, kilimo, ufugaji, usindikizaji na uandaaji na usambazaji katika hatua mbalimbali za mnyororo wa chakula”. Amesema Bw. Fimbo.
Aidha Bw. Fimbo ameongeza kuwa kazi ya kudhibiti usalama wa chakula nchini ni mojawapo ya jukumu la kisheria na la msingi la TFDA. Kwa kutambua na kuzingatia umuhimu wa usalama wa chakula katika kulinda afya ya jamii, TFDA imeweka mfumo thabiti wa udhibiti ili kuhakikisha chakula kinachozalishwa ndani ya nchi na kile kinachoingizwa nchini kinakidhi vigezo vya usalama na ubora ili walaji wasipate madhara ya kiafya.
Bw. Fimbo amemalizia kwa kusema kuwa Chakula salama ni jukumu la kila mmoja wetu ili kuleta mabadiliko chanya na kuhakikisha upatikanaji wa chakula salama kwa watanzania wote kwa lengo la kulinda afya ya jamii.