Msanii maarufu wa Bongo Fleva, Lady Jaydee akiimba nyimbo mbalimbali katika hafla ya kusherehekea mafanikio ya miaka 25 ya muziki wake iliyofanyika Juni 13, 2025 The Super Dome Masaki jijini Dar es Salaam.
………
Msanii maarufu wa Bongo Fleva, Lady Jaydee, ameweka wazi kuwa siri ya mafanikio yake katika sanaa ya muziki ni kuwa imara na kuamini katika kile anachokifanya.
Akizungumza Juni 13, 2025, jijini Dar es Salaam, katika hafla ya kusherehekea mafanikio ya miaka 25 ya muziki wake ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya uzinduzi wa album yake, Lady Jaydee amesema kuwa safari yake haikuwa rahisi, lakini aliweka juhudi kuhakikisha anafikia malengo.
Jaydee amesema kuwa kila msanii anapokuwa anaanza huwa na matumaini makubwa kuhusu mafanikio ya baadaye, ambapo juhudi, nguvu na kujituma ndizo zilizomsaidia kufanikisha ndoto zake na kufika alipo sasa.
Aidha, amewahimiza wasanii wa kike nchini, hasa mabinti, kujiamini kwani hilo ni jambo la msingi kwa yeyote anayetaka kudumu kwa muda mrefu katika tasnia ya muziki.
“Nawashauri mabinti waelewe kuwa kila kitu kinawezekana kama ukiwa na nia ya kweli ya kufanya,” amesema Jaydee.
Akizungumzia ratiba ya matukio ya maadhimisho ya miaka 25 ya muziki wake, Jaydee ameeleza kuwa Juni 20, 2025, watakuwa jijini Dodoma, na kisha Juni 27, watakwenda Mkoani Mwanza.
Vilevile, ametangaza kuwa anatarajia kutoa albamu mpya hivi karibuni, ambayo itaelezea historia ya maisha yake pamoja na muziki kwa ujumla.
Jaydee amesisisitiza kuwa muziki ni sanaa anayopenda kwa dhati, na ataendelea kuifanya katika maisha yake yote akiwa duniani.