Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Mahmoud Thabit Kombo (Mb.), ameongoza ujumbe wa Tanzania katika Mkutano wa Waratibu wa Utekelezaji wa Maazimio ya Jukwaa la Ushirikiano baina ya China na Afrika (FOCAC), unaofanyika tarehe 11-12 Juni 2025 jijini Changsha, China.
Mkutano huo umejadili utekelezaji wa Mpango Kazi wa FOCAC wa mwaka 2024 na kuidhinisha maeneo manne mapya ya matokeo, yakiwemo: kuimarisha biashara kati ya China na Afrika, utekelezaji wa miradi ya iliyochaguliwa katika ngazi ya majimbo, kuutangaza mwaka 2026 kuwa wa ushirikiano wa watu kwa watu, na azimio la mshikamano dhidi ya vita vya ushuru wa kibiashara vinavyoathiri mataifa yanayoendelea.
Katika hotuba yake ya ufunguzi, Waziri wa Mambo ya Nje wa China, Mhe. Wang Yi, ametangaza kuondoa ushuru wa forodha kwa bidhaa kutoka nchi zote 53 za Afrika zenye uhusiano wa kibalozi na China. Hatua hiyo inalenga kuongeza uingizaji wa bidhaa za Afrika katika soko la China na kuchochea ukuaji wa biashara.
Akiwasilisha salamu za Rais wa Jamhuri ya Watu wa China Mhe. Xi Jinping, Mhe. Wang Yi amesisitiza kuwa China inaupa kipaumbele cha juu ushirikiano wa kimkakati kati yake na Afrika, hasa katika kipindi hiki ambacho FOCAC inaadhimisha miaka 25 tangu kuanzishwa kwake.
Awali, katika Mkutano wa Kilele wa FOCAC wa mwaka 2024, China ilitangaza hatua 10 za ushirikiano zitakazopewa kipaumbele kwa kipindi cha 2025 hadi 2027, zikiwemo: kujifunza baina ya mataifa, ustawi wa biashara, ushirikiano wa viwanda, maendeleo ya miundombinu, afya, kilimo, ulinzi, maendeleo ya kijani, na ushirikiano wa watu kwa watu.
Ili kuendeleza utekelezaji wa malengo hayo, China iliahidi kutoa dola za Kimarekani bilioni 50, ambapo bilioni 29 ni kwa mikopo, bilioni 11 kwa misaada, na bilioni 10 kwa uwekezaji kutoka sekta za umma na binafsi.
Tanzania imenufaika na FOCAC kupitia miradi ya maendeleo katika sekta za afya, miundombinu, elimu, teknolojia, mifugo na utalii. Ushiriki wake unaimarisha nafasi ya nchi katika kukuza diplomasia ya kiuchumi na maendeleo jumuishi.