NA MWANDISHI WETU
TIMU ya soka ya waandishi wa habari, Taswa FC, imefungwa mabao 3-2 na kikosi cha Benki ya Stanbic katika mchezo wa kirafiki uliochezwa juzi kwenye Uwanja wa Gymkhana, Dar es Salaam.
Mchezo huo wa aina yake, uliandaliwa na Benki ya Stanbic kama sehemu ya kudumisha uhusiano na ushirikiano baina ya pande hizo mbili.
Katika mchezo huo uliohudhuriwa na wafanyakazi wa Benki ya Stanbic, wanahabari na wadau wengineo wa soka, Taswa FC ndiyo iliyokuwa ya kwanza kupata bao lililofungwa na Mbozi Katala, huku Zico George akifunga la pili.
Kwa upande wa Stanbic Bank, mabao yao yaliwekwa kimiani na Ally Masoud na Amrany Mlawa aliyecheka na nyavu mara mbili.
Kwa ujumla, mchezo huo ulikuwa mkali na wenye msisimko kwa dakika zote 90, ukitoa bonge la burudani kwa mashabiki wa soka waliojitokeza uwanjani hapo.
Baada ya mchezo huo, wachezaji wa timu zote mbili, wanahabari, wafanyakazi wa Stanbic Bank na wengineo, walijumuika kwa pamoja katika hafla ya chakula cha mchana iliyoambatana na vinywaji vya kila aina.
Akizungumza baada ya tukio hilo, meneja wa Taswa FC, Hussein Omari, aliipongeza Stanbic kwa tukio hilo, kuanzia mchezo huo uliokuwa wa aina yake, lakini pia kwa hafla fupi ya chakula cha mchana.
“Pongezi ziwaendee Benki ya Stanbic kwa kutukutanisha na kufurahi pamoja.
“Mchezo ulikuwa ni mzuri na wenye upinzani mkubwa, ila Stanbic FC washukuru Mungu kuna baadhi ya wachezaji wetu tishio hawakuweza kufika, akiwamo Mwenyekiti wetu, Majuto Omari ambaye yupo nje ya nchi kikazi. Pia, tuwashukuru kwa chakula na vinywaji kwani tumekula na kunywa hadi tumesaza,” alisema Hussein.
Kwa upande wake, Mkuu wa Kitengo cha Masoko na Mawasiliano wa Benki ya Stanbic, Desideria Mwegelo, aliwashukuru viongozi wa Taswa FC kwa kukubali kushiriki tukio hilo, lakini pia wanahabari wengineo waliojitokeza wka wingi.
“Wanahabari ni sehemu muhimu mno katika jamii hivyo sisi kama Stanbic Bank tumefarijika na umoja baina yetu licha ya kwamba tumewafunga Taswa FC,” alisema.
Akizungumza kutoka nchini Morocco alikokwenda kikazi, Mwenyekiti wa Taswa FC, Majuto, aliwapongeza Stanbic Bank kwa ushindi na kuwataka kuendeleza ushirikiano huo baina yao kwa manufaa ya pande zote mbili.