Mahakama Kuu ya Tanzania, Masijala Kuu ya Dar es Salaam, leo tarehe 6 Juni 2025 imetoa uamuzi muhimu unaobainisha mipaka ya mamlaka ya Mahakama za kiraia katika kushughulikia migogoro ya michezo, hususan soka. Uamuzi huo umetolewa na Jaji E.Y. Mkwizu katika shauri lililofunguliwa na mwanachama wa Yanga SC, Dkt. Samwel John Marwa, ambaye alitaka Mahakama iingilie kati mzozo wa kisoka kati ya klabu hiyo na Bodi ya Ligi Kuu Tanzania.
Dkt. Marwa, mkazi wa Iringa Mjini na mwenye kadi ya uanachama namba TZIRI03003030, alifungua kesi namba 9484 ya mwaka 2025 akiomba Mahakama:
- Ipe Yanga SC alama 3 na mabao 3 kwa madai kuwa Simba SC haikufika uwanjani katika mechi iliyopangwa tarehe 8 Machi 2025.
- Izuie Bodi ya Ligi kupanga tarehe nyingine kwa mchezo huo, ambao sasa umepangwa kuchezwa 15 Juni 2025.
Hata hivyo, katika uamuzi wake, Jaji Mkwizu alisisitiza kuwa Mahakama za kiraia hazina mamlaka ya kusikiliza migogoro ya soka, kwa mujibu wa Katiba ya TFF, kanuni za Ligi Kuu na Katiba ya Yanga SC yenyewe. Alifafanua kuwa masuala hayo yanapaswa kutatuliwa ndani ya mfumo rasmi wa michezo kupitia TFF, Kamati zake za maamuzi, na Mahakama ya Usuluhishi wa Michezo (CAS).
“Katiba za vyama na mashirikisho ya michezo zinawataka wanachama wake kuheshimu na kufuata utaratibu wa ndani wa utatuzi wa migogoro. Si jukumu la Mahakama kuingilia masuala ya kiutendaji ya michezo,” alisema Jaji Mkwizu.
Kwa msingi huo, Mahakama ilitupilia mbali madai ya Dkt. Marwa na kumuamuru kugharamia kesi hiyo.
Uamuzi huu unafuatia kile kilichotokea awali katika Mahakama ya Usuluhishi wa Michezo (CAS), ambapo Yanga SC walifungua shauri la kupinga uamuzi wa Bodi ya Ligi kuhusu mechi hiyo hiyo, na wakapoteza kwa “Technical Knockout” (TKO).
Kutokana na hali hiyo, juhudi zote za kuzuia mchezo huo kupitia njia za kisheria zimegonga mwamba – kuanzia CAS hadi Mahakama Kuu. Hili limeibua maswali kuhusu mustakabali wa maandalizi ya Yanga kuelekea mechi hiyo ya watani wa jadi.
Mjini Dar es Salaam, taharuki imeendelea kuongezeka miongoni mwa mashabiki na wanachama wa Yanga SC, huku baadhi ya sauti kutoka kwa viongozi wa klabu hiyo kama Mzee Msimu na watu wanaohusishwa na kundi lake, akiwemo Shabani Uda, zikielezwa kutoa matamshi yanayotafsiriwa kama vitisho dhidi ya kuchezwa kwa mechi hiyo.
Kwa sasa, Yanga SC imebakiwa na jukumu la kufanya maandalizi ya msingi – kuomba uwanja, kupanga kikosi na kutimiza masharti ya mechi hiyo. Iwapo wataamua kususia, huenda wakakumbana na adhabu kali kutoka TFF, ikiwemo kupokonywa alama au adhabu za kinidhamu kwa mujibu wa kanuni za TFF.