NA DENIS MLOWE IRINGA
MKURUGENZI wa shule za Star zilizoko mjini Iringa Jesca msambatavangu amesema wanatarajia kuanzisha chuo kitachofundisha mambo mbalimbali ya kijamii na kuendeleza vipaji.
Akizungumza na wanahabari Msambatavangu ambaye pia ni Mbunge wa Iringa mjini alisema kuwa chuo hicho kitatoa mafunzo katika sekta ya utalii, vipaji na afya ya akili katika upana zaidi.
Alisema kuwa chuo hicho kitawasaidia vijana wanaotaka kuelewa mambo ya utalii kwa undani zaidi, kutoa Mafunzo kwa wafanyakazi wa Hotel katika kujiongezea ufahamu zaidi katika mambo mbalimbali ya utalii na huduma za hotel .
Aidha alisema kuwa katika suala la vipaji watatoa elimu mbalimbali kwa vijana wenye vipaji mbalimbali mama ususi, mpira, kuimba na kuvipa misingi sahihi ya kukuza na kuendeleza vipaji vyao.
Msambatavangu ambaye ni amefanya mengi kwa ajili ya jamii mkoani hapa amesema katika suala la Afya ya akili watatoa elimu juu ya mambo mbalimbali kama mahusiano jinsi ya kupata mahusiano mema katika jamii, kumwondoa mtu katika misongo ya mawazo kwani ndio chanzo cha afya ya akili.
“Katika hili kuna umuhimu wa kujua chanzo cha afya ya akili vijana wengi wanaathirika kutokana msongo wa mawazo hivyo chuo chetu kitatoa elimu ya afya kwa upana zaidi.
Alisema chuo hicho kitakuwa na malipo kwa ajili ya kujiunga na mfumo mzima wa chuo na vitabu vya mafunzo vimeshakamilika na amefanikiwa kutunga vitabu viwili kwa ajili ya kutoa elimu kwa vijana.

