Na Sophia Kingimali.
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amezitaka halmashauri zote nchini kuanzisha vituo vya ukusanyaji wa taka ili kuendelea kutunza na kulinda mazingira.
Lakini pia ametoa rai kwa vijana kuchangamkia fursa zinazotokana taka taka ambazo zinazalishwa kwenye maeneo yao.
Maagizo hayo ameyatoa leo June 3,2025 wakati wa uzinduzi wa Mkakati wa Kitaifa wa Usimamizi wa Taka.
Amesema halmashauri zinapaswa kufanya kazi kwa karibu na Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira) kuwa na mipango ya pamoja ambayo inawashirikisha vijana katika mipango ya biashara ya kaboni.
Waziri Mkuu pia amesisitiza vijana kutazama changamoto za mazingira kama fursa za uvumbuzi lakini pia kuona umuhimu wa ushiriki wa jamii na kampeni za uhamasishaji wa umma.
“Kila Jumamosi, jamii zinapaswa kukusanyika kusafisha hospitali na maeneo yote ya umma hii inapaswa kuwa utamaduni wetu na jukumu la pamoja kwa mazingira yetu,” amesema.
Amesema serikali imejitolea kukuza nishati safi, na juhudi zinazoendelea za kupeleka umeme kwenye vijiji vyote ili kupunguza matumizi ya kuni.
Amesema serikali itaendelea kuongeza zaidi bajeti ya elimu ili kuboresha miundombinu kutoka shule za msingi hadi taasisi za juu za masomo ili kuhakikisha mazingira mazuri ya kujifunza kwa elimu ya mazingira.
“Tutaendelea Kuunga mkono ufikiaji wa ufadhili wa vijana, kwa kushirikiana na taasisi za kifedha ili kutekeleza miradi ya kijani ,” amesema.
Katika hatua nyingine waziri Mkuu amewataka vijana kutojihusisha na matukio yeyote yatakayopelekea kuvunja amani ya nchi yetu hasa kwenye kipindi hiki tunapoelekea uchaguzi mkuu.
“Tunashuhudia hata wageni wanaokuja nchini kusababisha machafuko ambayo hatupaswi, tunapaswa kulinda nchi kwa gharama yoyote,” amesema.
Kwa upande wake Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Khamis Hamza Khamis, amesema Tanzania inatarajia kuungana na Jumuiya ya Kimataifa katika kusherehekea Siku ya Mazingira Duniani Juni 5 ambapo kitaifa yatafanyikia Dodoma ambapo mwaka huu maadhimisho hayo yanazingatia ushiriki wa vijana katika kutunza mazingira.
Amesema kuwa serikali ilizindua kampeni ikihimiza kila kata kupanda miti milioni tano kila mwaka ili kupambana na ukataji miti na kulinda bioanuwai kwani lengo ni kupanda miti milion 1.5 ambapo bado halijafikiwa.
“Tunaandaa sheria, mikakati, na miongozo ya kukuza 3RS-kupunguza, kutumia tena, kuchakata tena. Taka, mara moja kuonekana kama uchafu, sasa taka ni chanzo cha utajiri, vijana wanapaswa kuchangamkia fursa katika uvumbuzi wa taka na biashara”,Amesema Khamis
Naye,Mwakilishi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Profesa Noah Mapula, amebainisha kuwa jukumu la chuo kikuu ni kuendelea kutengeneza wataalam wa mazingira na kuahidi kuendelea kuunga mkono utafiti na ushiriki wa vijana kwenye utunzaji wa mazingira.
Amesema mpaka sasa, kati ya tani milioni 14.4 hadi 20 za taka hutolewa kila siku nchini Tanzania hivyo mamlaka zinatakiwa kutumia teknolojia za kisasa ili kupunguza uchafuzi wa mazingira kwa angalau asilimia 50.