John Bukuku na Meleka Kulwa, Dodoma
Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Anthony Mtaka, amesema kuwa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) imetekelezwa kwa mafanikio makubwa mkoani humo, hususan katika sekta za afya, elimu na miundombinu.
Akizungumza leo Mei 29, 2025, katika Viwanja vya Jakaya Conversation Center wakati wa Mkutano Mkuu Maalum wa CCM unaofanyika kwa siku mbili, Mtaka alibainisha kuwa kila wilaya ya Njombe sasa ina vituo vya afya vilivyoimarishwa pamoja na stendi za mabasi, jambo linaloonyesha mafanikio ya wazi ya utekelezaji wa Ilani ya chama hicho tawala.
Mtaka alieleza kuwa Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imeonyesha dhamira ya kweli na weledi katika kutekeleza ahadi zake. Alisema kuwa ndani ya kipindi cha miaka mitano iliyopita, miradi mingi ya maendeleo imekamilika kwa mafanikio. Alitolea mfano wa kuanza kutekelezwa kwa ahadi ya ujenzi wa Ndaki ya Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) Njombe, ambapo eneo hilo tayari linaendelea kujengewa barabara ya zege baada ya fidia kwa wananchi kukamilika.
Aidha, Mtaka alisisitiza kuwa tofauti na miaka ya nyuma, wananchi sasa hawalazimiki tena kuchangia miradi ya maendeleo kwa kutumia rasilimali zao binafsi kama mifugo na mazao. Alisema serikali imechukua jukumu hilo kikamilifu, ambapo maboresho makubwa yamefanyika katika sekta ya afya na maji, na hivyo kupunguza vifo vya mama na mtoto sambamba na kumwezesha mama mjamzito kupata huduma za msingi kwa urahisi zaidi.
Kuhusu maendeleo ya kiuchumi, Mtaka alieleza kuwa serikali inaendelea kutoa mikopo ya asilimia 10 kwa vijana, wanawake na watu wenye ulemavu. Alisema kuwa Halmashauri ya Wilaya ya Njombe Vijijini pekee imetoa zaidi ya shilingi bilioni moja, na akatoa wito kwa wananchi kutumia fursa hizo kwa ajili ya kujiendeleza kiuchumi.
Akihitimisha hotuba yake, Mtaka alisema kuwa ndani ya miaka mitano ya uongozi wa Rais Dkt. Samia, Mkoa wa Njombe umefikia zaidi ya asilimia 85 ya upatikanaji wa huduma za msingi kama afya, elimu, kilimo, nishati na miundombinu. Alisisitiza kuwa mafanikio hayo yanapaswa kupongezwa na kuthaminiwa na wananchi wote, kwani CCM imetekeleza Ilani yake kwa mafanikio katika kila sekta.
Mkutano huo unatarajiwa kufikia hitimisho kesho, ukiendelea kujadili mafanikio pamoja na changamoto za utekelezaji wa Ilani ya CCM kwa kipindi kijacho.