Meneja wa RUWASA Wilaya ya Tandahimba Mkoani Mtwara Falaura Kikusa,akimuonyesha Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa Mwaka 2025 Ismail Ali Ussi ,mchoro wa mradi wa Kisima cha maji uliotekelezwa katika Kijiji cha Mivanga.
Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa Mwaka 2025 Ismail Ali Ussi,akikagua miundombinu ya mradi wa Kisima cha maji katika Kijiji cha Mivanga Wilaya ya Tandahimba Mkoani Mtwara kabla ya kuzindua mradi huo.
Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa Mwaka 2025 Ismail Ali Ussi,akizindua mradi wa Kisima cha Maji katika Kijiji cha Mivanga Wilaya ya Tandahimba Mkoani Mtwara,kulia Meneja wa Ruwasa Mkoa wa Mtwara Mhandisi Primy Damas
Picha no 315 Baadhi ya Wakazi wa Kijiji cha Mivanga Wilaya ya Tandahimba Mkoani Mtwara wakichota maji ya bomba baada ya Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa mwaka 2025 Ismail Ali Ussi(hayupo Pichani)kuzindua mradi wa kisima cha maji ikiwa ni mara ya kwanza katika Kijiji hicho kupata maji ya bomba tangu Uhuru.
Na Mwandishi Maalum,
Tandahimba
WAKALA wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini(Ruwasa)Wilaya ya Tandahimba Mkoa wa Mtwara,umetenga Sh. 452,500,000 zitakazotumika kuchimba visima vitano ili kumaliza kero ya Majisafi na salama katika Vijiji vya Mivanga,Lenyeje,Dinduma,Mchangani na Michenjele.
Meneja wa Ruwasa Wilaya ya Tandahimba Falaura Kikusa amesema,utekelezaji wa Visima hivyo mkakati maalum wa Rais Samia Suluhu Hassan, kupeleka maji kwenye maeneo yasiyo na huduma hiyo ili kutoa fursa kwa Wananchi kufanya shughuli za maendeleo badala ya kutumia muda mwingi kutafuta maji.
Kikusa amesema hayo,wakati akitoa taarifa ya mradi wa kisima kirefu kwa Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa Mwaka 2025 Ismail Ali Ussi kabla ya uzinduzi wa Programu Maalumu ya Uchimbaji Visima 900-5 kila Jimbo katika Kijiji cha Mivanga Wilayani humo.
Alisema,programu hiyo inatekelezwa kwa kutumia wataalam wa ndani(force account) na imepangwa kutekelezwa kwa muda wa Miezi sita kuanzia Mwezi Mei 2024 hadi Disemba 31 lakini kutokana na changamoto mbalimbali mpango huo utakamilika Mwezi Juni 2025 na hadi sasa utekelezaji wake umefikia asilimia 76.
“Ujenzi wa Miundombinu ya maji,usimikaji wa matanki ya kuhifadhi maji yenye ujazo wa lita 10,000 umefanyika katika vijiji viwili kati ya vitano ambavyo ni Mivanga na Lyenje huku usimakaji wa Pampu na mfumo wa nishati Jua umefanyika katika vijiji vinne vya Mivanga,Lyenje,Dinduma na Mchangani”alisema Kikusa.
Alisema, hadi sasa kazi zilifanyika kwa visima vyote vitano zinagharimu kiasi Sh.452,500.000 ambazo ni sawa na Sh.90,500,000 kwa kisima kimoja na kati ya fedha hizo Sh.124,106,686.40 zimelipwa.
“Chanzo cha fedha ya programu hii ni Lipa kwa Matokeo,Mfuko wa Taifa wa Maji na michango ya wadau mbalimbali wa maendeleo”alisema Kikusa.
Alisema,Program hiyo imesaidia kutoa ajira za muda mfupi kwa nguvu kazi ya Taifa yenye ujuzi wa kazi za ujenzi,upishi,udereva na upunguza adha ya maji kwa wakazi wa vijiji husika na utachochea muda wa kutosha katika shughuli za kiuchumi hususani kilimo na kudhibiti magonjwa ya milipuko ikiwemo kuhara na kipindupindu.
Kikusa alisema,katika Kisima cha Mivanga kina uwezo wa kuzalisha maji lita 372,000 kwa siku ambapo amewashukuru Wakazi wa vijiji hivyo kutoa maeneo yao bure yanayokadiriwa kuwa na thamani ya Sh.2,500,000.00 kwa ajili ya kutekeleza mradi huo.
Mbunge wa Jimbo la Tandahimba Katani Ahmed,ameishukuru Serikali kupitia Ruwasa kwa kutekeleza mradi wa visima visima katika Jimbo hilo ambavyo vimesaidia kupunguza changamoto ya upatikanaji wa huduma ya maji iliyokuwepo kwa muda mrefu katika vijiji hivyo.
Kwa upande wake Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa mwaka 2025 Ismail Ali Ussi,ameipongeza Serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuwajali na kuwathamini wakazi wa Jimbo la Tandahimba kwa kutafuta suluhisho la changamoto ya kudumu ya huduma ya majisafi na salama.
Ussi,amewaomba wananchi waliopata miradi ya visima kushirikiana na Serikali yao kutatua changamoto zilizopo na kutekeleza shughuli mbalimbali za maendeleo zinazolenga kuchochea Maendeleo yao na Taifa kwa ujumla.
Amewataka,wakazi wa kijiji cha Mivanga na maeneo mengine kuhakikisha wanatunza mradi huo na miundombinu yake ili uweze kudumu kwa muda mrefu na kuleta tija iliyokusudiwa katika kutatua kero ya maji ambayo ilisababisha kukosa muda wa kufanya shughuli zao za maendeleo.
Mkazi wa Kijiji cha Mivanga Asha Seleman alisema,mradi huo umemaliza adha ya majisafi na salama iliyokuwepo kwa muda mrefu na kupunguza gharama kubw
a za maisha kwa kununua ndoo moja ya maji ya lita 20 Sh.1,000.