Wanawake wamehimizwa kujielekeza katika malengo waliyojiwekea na wasikubali jitihada zozote hata kama zinatoka kwa watu wa karibu, ziwaondoe katika njia.
Hayo yamesemwa na Rais wa Jamhuri ya Namibia, Mhe. Dkt. Netumbo Nandi-Ndaitwah wakati akitoa mhadhara kwenye Chuo Kikuu cha Dar Es Salaam (UDSM) Mei 21, 2025.
Mhadhara huo uliobeba mada inayosema “Kuwahamasisha Wanawake Kuvunja Vizuizi vya kuelekea Nafasi za Uongozi” (Inspiring Women to break the Barriers in leadership positions), Rais Nandi-Ndaitwah alisema kuwa safari ya kuwawezesha wanawake ina historia ndefu, tokea enzi za kudai haki ya kupiga na kupigiwa kura, haki ya kumiliki, kuzalisha na kutumia mali na haki za kisiasa na kijamii.
Rais Nandi-Ndaitwah alisema kuwa usawa wa kijinsia ni muhimu ili kufikia maendeleo ya kweli na ndiyo maana Mkutano wa Dunia wa Wanawake uliofanyika Beijing mwaka 1995 ulijadili kwa kina masuala ya haki za wanawake na yeye akiwa mmoja wa wajumbe walioshiriki kwenye mkutano huo.
“Kufika ulipokusudia kwenda, kunahitaji kuwa na msimamo usioyumba na nidhamu ya hali ya juu, hivyo wanawake tunatakiwa kuzingatia masuala hayo ili kufikia malengo yetu” Alisema Rais Nandi-Ndaitwah.
Rais Nandi-Ndaitwah alisema matukio yanayotokea duniani na yanayowakuta wanawake wayachukulie kama masomo ya kufikia malengo yao badala ya kuwarejesha nyuma. Alisema udhalimu uliofanyika wakati wa ukoloni ambao ulisababisha yeye pamoja na wenzake kufungwa na kukimbia nchi, haukumkatisha tamaa isipokuwa aliyafanya kama daraja la kufikia malengo yake.
Alihitimisha hotuba yake kwa kusema kuwa wanawake wa leo wanaishi katika dunia yenye elimu bora na jamii iliyojaa ujuzi tofauti na miaka iliyopita, hivyo hakuna sababu au visingizio vya kuwazuia kufikia kwenye malengo yao.
Nao, viongozi wa chuo hicho wakiongozwa na Mkuu wa Chuo, Rais wa Awamu ya Nne, Mhe. Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete alisema kuwa mhadhara huo utabaki kuwa kumbukumbu kwa miaka mingi na kwamba Chuo kimefarijika kwa heshima iliyopewa na Rais Nandi-Ndaitwah.
Mhadhara huo ulihudhuriwa na watu mbalimbali wakiwemo Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Mhe. Prof. Adolf Mkenda; Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Prof. Palamagamba Kabudi; Mkuu wa Mkoa wa Dar Es Salaam, Mhe. Albert Chalamila, wanazuoni, wanachuo na wanafunzi wa shule za Sekondari.

