Dar es Salaam, Mei 20, 2025
Hatua ya Serikali ya kudhibiti matumizi holela ya fedha za kigeni katika malipo ya bidhaa na huduma ndani ya nchi imeanza kuonyesha mafanikio, ikiwa ni pamoja na kuimarika kwa thamani ya Shilingi ya Tanzania na kuongezeka kwa ukwasi wa fedha za kigeni katika soko.
Mkurugenzi wa Masoko ya Fedha wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Emmanuel Akaro, amesema hayo leo wakati wa semina kwa waandishi wa habari iliyofanyika katika ukumbi wa BoT jijini Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa Akaro, utekelezaji wa Kanuni za Matumizi ya Fedha za Kigeni ulioanza Machi mwaka huu umesaidia kuongeza ukwasi wa dola za Kimarekani katika soko kutoka wastani wa dola milioni 40 hadi milioni 69 kwa siku ndani ya mwezi mmoja.
“Watu waliokuwa wakifanya miamala kwa kutumia fedha za kigeni sasa wanalazimika kubadilisha kwanza na kulipa kwa shilingi, jambo ambalo limeongeza nguvu ya sarafu yetu ya ndani,” alisema Akaro.
Aliongeza kuwa fedha za kigeni zinazopatikana kwa sasa zimeongezeka kwa kiasi kikubwa ikilinganishwa na kipindi kama hiki mwaka jana ambapo ilikuwa wastani wa dola milioni 30 kwa siku, huku mwaka huu ikiwa karibu dola milioni 70.
Akaro alisema kuwa Benki Kuu inaendelea kusimamia kwa karibu utekelezaji wa sera zake ili kudhibiti mfumuko wa bei na kuhakikisha mazingira ya kifedha yanabaki kuwa tulivu, ambapo kwa sasa mfumuko wa bei umebaki katika kiwango cha asilimia 3.1.
“Mpaka sasa tumeshatoa dola milioni 130 kwenye soko mwaka huu ili kuhakikisha upatikanaji wa fedha za kigeni unatosheleza, lakini pia kuhakikisha kwamba miamala ya ndani inafanyika kwa shilingi kama sheria inavyoelekeza,” alisema.
Kwa mujibu wa Kanuni za Matumizi ya Fedha za Kigeni (GN. Na. 198 ya mwaka 2025), zilizochapishwa Machi 28, 2025 chini ya Sheria ya Benki Kuu ya Tanzania, wananchi na wafanyabiashara wote wanatakiwa kutumia shilingi ya Tanzania katika manunuzi ya bidhaa na huduma ndani ya nchi.
Kanuni hizo, zilizotangazwa na Waziri wa Fedha Dkt. Mwigulu Nchemba, zinalenga kudhibiti utumiaji holela wa sarafu za kigeni na kuongeza uthabiti wa mfumo wa fedha wa nchi.