Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Mahmoud Thabit Kombo, amesema kuwa Sera mpya ya Mambo ya Nje ya mwaka 2001 (Toleo la mwaka 2024) inalenga kuiimarisha Tanzania kimataifa kwa kutumia diplomasia makini na shirikishi ili kulinda na kutetea maslahi ya taifa.
Akizungumza leo Jumatatu, Mei 19, 2025, katika uzinduzi wa sera hiyo uliofanyika kwenye Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere, Balozi Kombo amesema Tanzania ina dhamira ya kuendelea kuwa kisiwa cha amani, utulivu na umoja, na kuwa na mchango mkubwa katika ulinzi wa amani duniani.
“Sera hii ni nyenzo ya kimkakati kuhakikisha Tanzania inaendana na mazingira yanayobadilika kwa kasi duniani, huku ikiimarisha ushirikiano wa kimataifa kwa tija zaidi,” amesema.
Waziri Kombo amefafanua kuwa sera hiyo inaiwezesha Tanzania kuwa na sauti yenye ushawishi katika uhusiano wa kibiashara na kimataifa, sambamba na kuchochea ushiriki wa nchi katika masuala ya kiuchumi duniani.
Aidha, ameeleza kuwa mchakato wa maboresho ya sera hiyo ulihusisha ushiriki mpana wa wananchi kutoka maeneo mbalimbali nchini, kufuatia maelekezo ya Rais Samia Suluhu Hassan, jambo linaloifanya kuwa sera shirikishi na jumuishi.
“Ni matarajio yetu kuwa malengo yaliyowekwa katika Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050, ikiwemo kufikia uchumi wa kipato cha kati cha juu, yatatimia kwa kutumia sera hii kama mwongozo wa kimataifa wa utekelezaji,” amesema Balozi Kombo.
Sera hii mpya inajengwa juu ya msingi wa kulinda maslahi ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuzingatia mazingira ya sasa ya kisiasa, kijamii, kiuchumi na kiusalama katika ngazi ya kikanda na kimataifa.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akizindua Sera ya Mambo ya Nje ya mwaka 2001 Toleo la Mwaka 2024 katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC) Jijini Dar es Salaam tarehe 19 Mei, 2025.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akiwa na viongozi mbalimbali pamoja na wageni mbalimbali kwenye hafla ya uzinduzi wa Sera ya Mambo ya Nje ya mwaka 2001 Toleo la Mwaka 2024 katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC) Jijini Dar es Salaam tarehe 19 Mei, 2025.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akitembelea mabanda ya maonesho kabla ya kuzindua Sera ya Mambo ya Nje ya mwaka 2001 Toleo la Mwaka 2024 katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC) Jijini Dar es Salaam tarehe 19 Mei, 2025.