Dkt Charles Mwamwaja Kamishna wa Sekta ndogo ya Fedha Wizara ya Fedha na Mipango akiwasilisha mada katika semina ya wahariri wa vyombo vya habari na waandishi wa habari kuhusu utoaji elimu ya Sera, Sheria, Kanuni za biashara ya huduma ndogo za fedha inayofanyika kwenye hoteli ya Nashera mjini Morogoro.
Bi. Dionisia Mjema Kaimu Kamishna Msaidizi Idara ya Maendeleo ya Sekta ya Fedha Wizara ya Fedha akifafanua jambo wakati alipokuwa akiwasilisha mada katika semina hiyo leo kwenye Hoteli ya Nashera mjini Morogoro.
MKuu wa Mawasiliano na Msemaji Mkuu wa Wiazara ya Fedha na Mipango Bw. Ben Mwaipaja akitolea ufafanuzi katika baadhi ya mambo yaliyojitokeza katika semina hiyo.
Bw. Shanil Mayosa Mwanasheria kutoka tume ya Ushirika ni miongozi mwa wataalamu waliotoa mada kwa wahariri wa vyombo vya habari na waandishi leo mjini Morogoro.
Bi. Ng’waka Mong’ateko Meneja Msaidizi Idara ya Huduma Ndogo za Fedha na Maduka ya Kubadilishia Fedha za Kigeni kutoka Benki Kuu ya Tanzania (BoT) akiwasilisha mada katika semina hiyo
Wadau mbalimbali wakiwa katika semina hiyo.
Baadhi ya wahariri wa vyombo vya habari mbalimbali na waandishi wa habari wakifuatilia mjadala katika semina hiyo.
Kutoka kushoto ni Kamishna anayesimamia Sekta Ndogo ya Fedha kutoka Wizara ya Fedha , Dkt. Charles Mwamaja, Bi. Dionisia Mjema Kaimu Kamishna Msaidizi Idara ya Maendeleo ya Sekta ya Fedha Wizara ya Fedha na Meneja Msaidizi wa Idara ya Uhusiano wa BOT, Vicky Msina pamoja na washiriki wengine wa semina hiyo wakifuatilia mada mbaimbali zilizokuwa zikiendelea.
……………………………………………………
KATIBU MKuu Wizara ya Fedha na Mipango, Doto James, amesema Sekta Ndogo ya Fedha ni miongoni mwa sekta muhimu katika uchumi wa nchi.
Alisema sekta hiyo inatoa huduma za fedha kwa wananchi wa kipato cha chini na kati ambazo zinachangia kuinua uchumi na kuongeza kipato.
Kamishna anayesimamia Sekta Ndogo ya Fedha kutoka Wizara hiyo, Dkt. Charles Mwamaja aliyasema hayo mkoani Morogoro kwa niaba ya James kwenye semina iliyoshirikisha Wahariri wa vyombo mbalimbali nchini ikihusu utoaji elimu ya Sera, Sheria, Kanuni za biashara ya huduma ndogo za fedha.
Alifafanua kuwa, kwa mujibu wa utafiti wa Finscope wa mwaka 2017, asilimia 55.3 ya nguvukazi ya Taifa wanapata huduma za fedha kutoka taasisi za huduma ndogo za fedha
Kutokana na umuhimu wa Sekta hiyo, Serikali kupitia Wizara ya Fedha na Mipango ilifanya mapitio ya Sera ya Taifa ya Huduma Ndogo za Fedha ya Mwaka 2000 na kutunga Sera ya Taifa ya Huduma Ndogo za Fedha ya Mwaka 2017.
Sera hiyo pamoja na mambo mengine, imeelekeza kutungwa kwa Sheria mahsusi ya kusimamia na kuendeleza sekta ya huduma ndogo ya fedha ili kuondoa changamoto za kisheria zilizokuwepo ambazo ziliathiri usimamizi, udhibiti na ustawi wa sekta hiyo.
Miongoni mwa changamoto hizo ni pamoja na taasisi za huduma ndogo za fedha kutoa mikopo kwa wananchi kwa vigezo, masharti magumu hivyo kusababisha madhara kwa wananchi.
Madhara hayo ni pamoja na viwango vikubwa vya riba, tozo na kukosekana kwa uwazi wa masharti ya mikataba ya mikopo, utoaji holela wa mikopo unaosababisha limbikizo la madeni kwa wateja.
Aliyataja madhara mengine ni utaratibu usiofaa wa ukusanyaji madeni unaosababisha wananchi kupoteza mali zao, kujitokeza kwa baadhi ya wananchi wasio waaminifu wanaotumia mwanya wa kutokuwepo sheria mahsusi kutoa huduma ndogo za fedha.
Mashara mengine ni kuwepo kwa baadhi ya taasisi za huduma ndogo za fedha zisizotoa gawio au faida kwa wanachama, wateja wanaoweka fedha kati ya asilimia 25 hadi 30 kama dhamana ya mikopo, ukosefu wa takwimu ama taarifa sahihi za uendeshaji taasisi za watoa huduma ndogo za fedha.
James alisema pia kukosekana takwimu, taarifa tajwa husababisha Serikali kutojua mchango wa sekta ndogo ya fedha katika uchumi wa Taifa, ukosefu wa utaratibu wa kuwalinda watumiaji wa huduma ndogo za fedha.
Pia kuwepo kwa mianya ya utakasishaji fedha haramu kutokana na taasisi za huduma ndogo za fedha kutokuwa na utaratibu wa kisheria unaozitaka kutekeleza matakwa ya Sheria ya Udhibiti wa Utakasishaji wa Fedha Haramu.
Ili kutatua changamoto zinazoikabili Sekta Ndogo ya Fedha kama nilivyobainisha katika maelezo ya awali, Serikali ilitunga Sheria ya Huduma Ndogo za Fedha ya mwaka 2018 (The Microfinance Act, 2018).
Lengo la sharia hiyo, kwanza ni kuzitambua taasisi za huduma ndogo za fedha katika madaraja manne, daraja la kwanza ni taasisi za huduma ndogo za fedha zinazopokea amana, pili taasisi zisizopokea amana wakiwemo wakopeshaji binafsi, watoa huduma kwa njia ya kielekroniki, kampuni za mikopo.
Daraja la Tatu ni vyama vya Ushirika wa Akiba na Mikopo (SACCOS) na daraja la nne ni vikundi vya kijamii vya huduma ndogo za fedha kama VICOBA, VSLA.
Sheria hiyo imeanza kutumika rasmi Novemba Mosi, 2019, pamoja na mambo mengine imeainisha kuwa ifikapo Oktoba 31, mwaka huu, kila mtoa huduma ndogo za fedha lazima awe amekata leseni au kusajiliwa kufanya biashara ya huduma ndogo za fedha kwa kuzingatia daraja husika.
“Tayari zimeandaliwa kanuni mahsusi na kanuni za jumla kwa ajili ya kutekeleza majukumu ya Waziri ya kisera, kuhamasisha, usimamizi na kuendeleza sekta ndogo ya fedha,” alisisitiza.
Kwa upande wake, Dkt. Mwamaja alisema sekta hiyo imepitia changamoto nyingi ambazo zilisababisha Serikali kupitia Wizara ya Fedha na Mipango kufanya mapitio ya Sera ya Taifa ya Huduma Ndogo za Fedha ya Mwaka 2000 na kutunga Sera ya Taifa ya Huduma Ndogo za Fedha ya Mwaka 2017.
Lengo la kuwepo kwa Sera, Sheria na Kanuni hizo ni kuweka mazingira wezeshi ya usimamizi, uendelezaji sekta ya huduma ndogo za fedha nchini ili kuondoa changamoto zilizokuwepo katika sekta hiyo iweze kutoa mchango mkubwa ili kukuza uchumi na kuondoa umaskini.
“Semina hii imeandaliwa na Wizara ya Fedha ikishirikiana na wadau wengine wakiwemo Ofisi ya Raisi- TAMISEMI, Benki Kuu ya Tanzania, Tume ya Maendeleo ya Ushirika (TCDC) na Baraza la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC), Mfuko wa Kuendeleza Sekta ya Fedha (FSDT),” alisema.