Dar es Salaam 19 Mei, 2025

Rais wa Jamhuri ya Namibia, Mhe. Dkt. Netumbo Nandi-Ndaitwah anatarajia kufanya

Ziara ya Kiserikali ya siku mbili nchini Tanzania kuanzia tarehe 20 hadi 21 Mei, 2025 kwa

mwaliko wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Taarifa iliyotolewa na  Naibu Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu  Shaaban Kissu imesema Hii ni ziara ya kwanza ya Rais Dkt. Nandi-Ndaitwah nchini Tanzania tangu aapishwe kuwa

Rais wa Jamhuri ya Namibia tarehe 21 Machi 2025 na inalenga kukuza ushirikiano wa

kisiasa, kiuchumi na kijamii, ikiwemo katika nyanja za biashara, uwekezaji na elimu.

Tanzania na Namibia zimejenga uhusiano wa muda mrefu wa kidugu na kidiplomasia,

hivyo ziara hii itafungua fursa mpya za ushirikiano zitakazowawezesha wananchi wa nchi zote mbili kunufaika kiuchumi.

Rais Dkt. Nandi-Ndaitwah atapokelewa Ikulu ya Dar es Salaam na mwenyeji wake, Rais

Dkt. Samia ambapo viongozi hao wawili wanatarajia kuwa na mazungumzo ya uwili na

kisha kuongoza mazungumzo rasmi baina ya nchi hizo mbili na baadae kuzungumza na waandishi wa habari.

Aidha, akiwa nchini Tanzania, Rais Dkt. Nandi-Ndaitwah atatembelea Kituo cha Urithi wa

Ukombozi wa Afrika pamoja na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, kama sehemu ya

kuthamini mchango wa kihistoria wa Tanzania katika harakati za ukombozi barani Afrika

na pia kukuza ushirikiano wa kielimu na kiutamaduni kati ya Namibia na Tanzania.

Rais Dkt. Netumbo Nandi-Ndaitwah anatarajia kuhitimisha ziara yake tarehe 21 Mei, 2025.