Na Ashrack Miraji Fullshangwe Media
Mkuu wa Wilaya ya Lushoto, Zephania Sumaye, amekabidhi reflector 1,000 kwa vijana wa bodaboda ikiwa ni sehemu ya kampeni ya kuhamasisha ushiriki wa vijana katika uandikishaji wa wapiga kura kwa ajili ya Uchaguzi Mkuu ujao. Katika tukio hilo, vijana 200 kati yao tayari wamejiandikisha kupiga kura, wakichochewa na kampeni hiyo ya hamasa inayofanyika wilayani Lushoto, mkoani Tanga.
Hafla hiyo ilifanyika katika Uwanja wa Nyerere Square ambapo DC Sumaye aliwataka vijana kujitokeza kwa wingi kujiandikisha ili waweze kushiriki kikamilifu katika uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani unaotarajiwa kufanyika mwezi Oktoba mwaka 2025. Alisema lengo kuu la kugawa reflector hizo ni kuwapa vijana motisha na kuwahimiza kutimiza wajibu wao wa kikatiba kama raia.
Katika mkutano huo wa hadhara, vijana zaidi ya 200 waliokuwepo ambao bado hawakuwa wamejiandikisha, walieleza kuwa wameguswa na ujumbe wa Mkuu wa Wilaya na wako tayari kujiandikisha mara moja. Walieleza kuwa ni mara ya kwanza kuona uongozi ukikaribia jamii kwa njia ya vitendo na kuwahusisha moja kwa moja katika masuala ya kitaifa.
DC Sumaye alisisitiza kuwa reflector hizo pia zitasaidia katika kuwatambua madereva wa bodaboda maeneo mbalimbali ya wilaya hiyo. Kila dereva anatakiwa kuwa na namba maalum ya utambulisho, jambo ambalo litasaidia katika masuala ya ulinzi na usalama, hasa pale panapotokea changamoto zinazohitaji kufuatiliwa kwa haraka.
Aidha, Mkuu huyo wa wilaya aliwahimiza viongozi wa vikundi vya bodaboda kushirikiana kwa karibu na ofisi yake katika kuhakikisha kuwa vijana wanapata elimu ya uraia, hususan kuhusu umuhimu wa kushiriki katika uchaguzi na michakato mingine ya kidemokrasia.
Vijana walioshiriki hafla hiyo walimpongeza DC Sumaye kwa kuwajali na kuwathamini, huku wakiahidi kuwa mabalozi wa kuwahamasisha wenzao waliobaki kujiandikisha kabla ya muda wa uandikishaji kumalizika. Walisema hatua hiyo imeonyesha wazi kuwa serikali inatambua mchango wa vijana katika maendeleo ya taifa.
Kwa upande mwingine, baadhi ya viongozi wa jamii waliohudhuria tukio hilo walipongeza juhudi za serikali ya wilaya na kushauri kampeni kama hiyo ifanyike pia katika maeneo ya vijijini ambako uhamasishaji bado ni mdogo, ili kuhakikisha hakuna kijana anayekosa haki ya kupiga kura.