Tanzania imeweka bayana dhamira yake ya kuwa kinara wa mapinduzi ya elimu na teknolojia barani Afrika, kupitia ushiriki wake kwenye Kongamano la e-Learning Africa lililofanyika jijini Dar es Salaam Mei 9, 2025.
Makamu wa Pili wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Mhe. Hemed Suleiman Abdulla, amesema kuwa Tanzania ipo tayari kushirikiana na wawekezaji, wafanyabiashara na taasisi mbalimbali za kimataifa katika nyanja za kiteknolojia na elimu ili kuharakisha maendeleo ya nchi na bara la Afrika kwa ujumla.
“Kupitia teknolojia, tunaweza kuleta mabadiliko chanya ya kijamii na kiuchumi. Tanzania iko tayari kuwa sehemu ya mabadiliko hayo,” alisema Mhe. Hemed katika hotuba yake ya ufunguzi wa kongamano hilo linalowakutanisha wadau wa elimu kutoka mataifa mbalimbali.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda, alieleza kuwa kongamano hilo ni fursa adhimu kwa nchi za Afrika kuangalia upya namna bora ya kufundisha kwa kutumia nyenzo za kidijitali. Alisema mwongozo uliotolewa utaiwezesha Tanzania na nchi nyingine kuhimarisha mifumo yao ya elimu na kuchochea maendeleo ya kisasa.
Kwa upande wake, Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Jerry Silaa, aliweka wazi kwamba Tanzania inaendelea kutekeleza kwa vitendo Mpango wa Miaka 10 wa Uchumi wa Kidijitali uliopitishwa na Rais Samia Suluhu Hassan, ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa Sera ya Taifa ya TEHAMA ya mwaka 2016.
Alitaja ujenzi wa miundombinu ya TEHAMA, ikiwa ni pamoja na usambazaji wa mtandao wa intaneti na ujenzi wa minara 758 ya simu, kama sehemu ya jitihada hizo. Aidha, alitoa pongezi kwa Wizara ya Elimu kwa maandalizi bora ya kongamano hilo ambalo limeiweka Tanzania kwenye ramani ya kimataifa ya elimu na teknolojia.