Mwenyekiti wa Bodi ya Faida Fund, Abdulrazaq Badru akizungumza na wanahisa katika mkutano wa mwaka uliofanyika kwenye ukumbi wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam leo Mei 3, 2025.
Sephania Solomon Kaimu Mkurugenzi Watumishi Housing Investment WHI akifafanua baadhi ya mambo katika mkutano huo wa mwaka wa wanahisa.
Paschal Massawe Mkurugenzi wa Fedha na Utawala Watumishi Housing Investment WHI akitoa taarifa ya fedha ya mfuko huo katika mkutano wa mwaka wa wanahisa.
………………
Dar es Salaam – Mfuko wa Uwekezaji wa Faida Fund unaosimamiwa na Watumishi Housing Investment (WHI) umeonesha mafanikio makubwa kwa mwaka 2024, na sasa unajipanga kutanua wigo wa wanachama kwa kuwafikia wajasiriamali, wakiwemo waendesha bodaboda, ili kushiriki katika uwekezaji unaowaletea tija.
Akizungumza leo Mei 3, 2024, katika Mkutano Mkuu wa Pili wa mfuko huo uliofanyika katika Ukumbi wa JNICC, Mwenyekiti wa Bodi ya Faida Fund, Abdulrazaq Badru, amesema ongezeko la wanachama kutoka 2,041 mwaka 2023 hadi 4,806 kwa mwaka 2024 limechangia kuimarika kwa thamani ya mfuko huo hadi kufikia Sh25.97 bilioni kutoka Sh15.6 bilioni, sawa na ongezeko la asilimia 67.
“Nimepokea na kupitia taarifa ya fedha ya Juni 30, 2024, na nina furaha kusema utendaji wa mfuko ulikuwa mzuri. Faida kwa wawekezaji wetu ilikuwa ya kuridhisha ikilinganishwa na vigezo vya utendaji,” alisema Badru.
Badru alibainisha kuwa mafanikio hayo yametokana na kuongezeka kwa imani ya wawekezaji, juhudi za kutoa elimu ya kifedha na usimamizi madhubuti, hali inayotoa fursa kwa mfuko kuwajumuisha watu wengi zaidi kutoka sekta isiyo rasmi.
Kwa upande wake, muelimishaji wa masuala ya fedha wa mfuko huo, Amina Ramadhani, alitoa wito kwa wanachama kuweka urithi sahihi kwa manufaa ya familia zao. “Ni vyema wanachama wakatafakari kwa makini ni nani wa kurithi mafao yao ili kuepusha migogoro iwapo watatoweka,” alisema.
Naye Allan Mwaigaga, mwekezaji kutoka Mkoa wa Mbeya, alipendekeza juhudi za makusudi zielekezwe kwa jamii za vijijini na sekta binafsi. “Wengi wetu ni Watumishi wa Umma, lakini kule nilikotoka wapo wajasiriamali wanaoweza kujiunga ikiwa watapatiwa elimu sahihi,” alisema.
Katika hitimisho la mkutano huo, Badru alitangaza kuwa mkutano mkuu ujao wa wanachama wa Faida Fund utafanyika Aprili 18, 2026.