Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ametoa wito kwa Watanzania kuulinda na kuudumisha Muungano wa Tanganyika na Zanzibar kwa nguvu zao zote, akisisitiza kuwa ni tunu ya kipekee inayopaswa kuenziwa kwa vitendo, umoja na mshikamano wa kitaifa.
Akihutubia taifa kuelekea maadhimisho ya miaka 61 ya Muungano, Rais Samia amesema mwaka huu wa maadhimisho unaangukia katika kipindi muhimu kwa taifa, ambapo Watanzania watafanya uchaguzi mkuu kuchagua viongozi wa ngazi mbalimbali, ikiwemo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Rais wa Zanzibar, Wabunge, Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi na Madiwani.
“Mwaka wa 61 wa Muungano wetu umeangukia kwenye mwaka tunaokabiliwa na jambo kubwa la kidemokrasia nchini… Ni matumaini yangu kuwa tutaendelea kudumisha sifa ya nchi yetu kuwa ni kitovu cha amani na nchi ya kidemokrasia iliyojengeka juu ya misingi ya uhuru na haki,” alisema Rais Samia.
Rais amesisitiza kuwa Serikali imejipanga kikamilifu kuhakikisha kuwa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi inapata mahitaji yote kwa wakati, na mazingira ya uchaguzi yatakuwa ya utulivu, amani, na yataruhusu uchaguzi huru na wa haki. Ametoa wito kwa wananchi kujitokeza kwa wingi kushiriki katika hatua zote za mchakato wa uchaguzi – kuanzia kujiandikisha, kugombea, hadi kupiga kura.
Aidha, Rais Samia amewataka viongozi na wanachama wa vyama vya siasa kufuata sheria, taratibu na miongozo ya uchaguzi ili kulinda utulivu wa kitaifa. “Kamwe tusiruhusu uchaguzi uwe chanzo cha migogoro, chuki, mivutano na uvunjifu wa amani… Hakuna aliye juu ya sheria,” alionya.
Akihitimisha hotuba yake, Rais Samia amewakumbusha Watanzania kuhusu wajibu wao katika kuulinda na kuendeleza Muungano. Amesema waasisi wa Muungano, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na Sheikh Abeid Amani Karume, waliuishi Muungano kwa maneno na matendo yao, hivyo ni jukumu la kila Mtanzania kuendeleza tunu hiyo kwa msingi wa udugu, uzalendo na mshikamano.
“Kesho, tunapofikia kilele cha maadhimisho ya miaka 61 ya Muungano wetu, katika Mikoa na Wilaya zetu Tanzania nzima, nitumie fursa hii kuwatakieni Watanzania wote Maadhimisho mema ya Miaka 61 ya Muungano,” alihitimisha.