*Asisitiza CCM daima itaenzi misingi ya Nyerere
Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Balozi Dkt. Emmanuel John Nchimbi amesema CCM itahakikisha inateua wagombea wazuri wanaokubalika kwa wapiga kura, akiwataka wajumbe wa vikao vya kura za maoni kusikiliza maoni ya wananchi wanapoenda kupiga kura.
Halikadhalika, Balozi Nchimbi ametoa wito kwa Watanzania wote, hususan wenye sifa za kupiga kura, kuwapatia maoni yao wajumbe wa vikao hivyo vya uchujaji wagombea wa CCM, ili wanapoenda kupiga kura za maoni wachague wagombea wanaokubalika katika jamii pana ya wapiga kura wa Uchaguzi Mkuu utakaofanyika Oktoba, mwaka huu.
Balozi Nchimbi amesema hayo alipozungumza na wananchi wa Butiama, katika eneo la Nyamisisi, aliposimama kuwasalimia wakati akiendelea na ziara ya kikazi ya siku tano katika Mkoa wa Mara, leo Alhamis tarehe 24 Aprili, 2025, ikiwa ni siku ya tatu ya ziara hiyo.
“Napenda kuwahakikishia kuwa CCM daima itaendelea kujinasibisha na misingi ya Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere. Kamwe hatutaacha hilo. Mwalimu alituachia wosia muhimu sana kuwa bila CCM imara, nchi itayumba. Ndiyo maana muda wote hatuachi matatizo ya kimfumo, kimuundo wala kiuongozi yaisumbue CCM maana nchi itayumba,” alisema Balozi Nchimbi.
Ameongeza kuwa mojawapo ya misingi hiyo ya Nyerere, ambayo ndiyo pia iliyoasisi CCM kuanzia TANU, ni pamoja na chama hicho kuwa kimbilio na sauti ya wanyonge, kuwatumikia wananchi wote bila ubaguzi kwa sababu binadamu wote ni sawa, pamoja na kuimarisha demokrasia.
Katika hatua nyingine, Balozi Nchimbi aliwaambia wananchi kuwa misingi hiyo hiyo ndiyo itakayoendelea kukiongoza CCM katika kusikiliza maoni ya wananchi ili kupata wagombea wanaokubalika kugombea nafasi za udiwani, uwakilishi na ubunge.
“Kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka huu, tumeongeza idadi ya wapiga kura kwenye vikao vya kura za maoni, hivyo watakuwa kielelezo kusaidia CCM kupata picha kubwa ya nje kupitia wajumbe hao. Natoa wito kwa Watanzania wote, siku wakiona wajumbe wa CCM wanakwenda kupiga kura za maoni katika maeneo yao, wawaambie tunamtaka fulani,” alisisitiza.
“Natoa wito kwa wajumbe wa CCM pia kuhakikisha wanawasikiliza wananchi. Wananchi wanajua viongozi wanaoweza kuwatumikia. Lazima tuwasikilize wananchi. Wajumbe sikilizeni kauli za wananchi. Wapeni kile wanachokitaka, tuchague watu kwa sifa za uongozi. Tusichague mtu kwa ukabila, wala dini, wala utajiri wake. WanaCCM timizeni wajibu wenu kwa kukataa hayo ili CCM ipate wagombea wanaokubalika kwa watu,” aliongeza.
Mapema kabla ya mkutano huo, Balozi Nchimbi alitembelea na kukagua maendeleo ya mradi wa Chuo Kikuu cha Mwalimu Nyerere cha Kilimo na Teknolojia (MJNUAT) kinachojengwa Butiama na kuweka jiwe la msingi kwa ajili ya ujenzi wa Ofisi ya CCM wilayani humo.
Aidha, Katibu Mkuu huyo wa CCM alitumia nafasi hiyo kuendelea kuwahamasisha wananchi kujiandaa kuboresha taarifa zao kwenye Daftari la Kudumu la Wapiga Kura kwa ajili ya kushiriki Uchaguzi Mkuu wa Oktoba mwaka huu.