Waziri wa Maji, Mhe. Jumaa Aweso (Mb) amewataka watumishi wa Wizara ya Maji kuongeza zaidi bidii katika kazi na kutumia weledi kwa kuzingatia Sheria, Kanuni na Taratibu za utumishi wa umma.
Waziri Aweso amesema bidii katika kazi kwa watumishi wa Wizara ya Maji ndiyo siri kubwa ya mafanikio na maendeleo ya Sekta ya Maji nchini, akisisitiza kuwa bidii pamoja na ushirikiano vinaleta tija katika taasisi.
Mhe. Aweso amezungumza hayo kwa wajumbe wa Mkutano wa Baraza la Wafanyakazi uliokuwa na kaulimbiu “Baraza la Wafanyakazi ni Chombo Muhimu cha Kuleta Mahusiano Mazuri Mahala pa Kazi, Tushirikiane Kutunza Azma ya Kumtua Mama Ndoo Kichwani”, inayosisitiza umuhimu wa umoja na ushirikiano kupitia baraza hilo.
“Niwaase watumishi wa Wizara ya Maji fanyeni kazi kwa bidi na upendo, mpeane moyo na kuneneana mema kila mmoja. Msiwe na tabia ya kufanyiana hiana na fitina kwa sababu baadala ya kuwasaidia, itakuwa sumu kubwa katika utendaji wenu wa kazi na kuwa changamoto kufikia malengo ya taasisi.
“Ninaamini watumishi wakiwa kwenye mazingira mazuri ya kazi, watafanya kazi nzuri. Hivyo, tukiwa viongozi wa Wizara ya Maji tutaendelea kuimarisha na kuboresha mazingira ya kazi kwa maendeleo ya Sekta ya Maji”, Waziri Aweso amesema.
Pia, amewataka viongozi wa Baraza la Wafanyakazi la Wizara ya Maji kuzingatia haki za watumishi na ustawi wao kwa kuwa wao ndio nyenzo kuu ya taasisi katika kufanikisha malengo yake.
Awali, Katibu Mkuu na Mwenyekiti wa Baraza la Wafanyakazi la Wizara ya Maji, Mhandisi Mwajuma Waziri amewashukuru watendaji wote wa Sekta ya Maji kwa utendaji wao mzuri katika kufanikisha utekelezaji wenye mafanikio wa Bajeti ya mwaka 2024/25.
Mhandisi Mwajuma amesema watumishi wote wa Wizara ya Maji-Makao Makuu pamoja na taasisi zake zote za Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA), Mamlaka za Maji, Mfuko wa Taifa wa Maji, Bodi za Maji za Mabonde na Chuo cha Maji wamekuwa sehemu ya mafanikio hayo kwa utendaji nzuri wa kazi katika kufanikisha na kuyafikia malengo ya kisekta kwa mwaka wa fedha unaoisha.
Aidha, mkutano huo wa Baraza la Wafanyakazi unaofanyika kila mwaka ulikuwa na ajenda kadhaa zikiwemo uchaguzi wa Katibu wa Baraza la Wafanyakazi ambapo Yasin Lusheke, Mchumi Mwandamizi kutoka Idara ya Sera na Mipango kashinda nafasi hiyo. Pamoja na wasilisho la utekelezaji wa Mpango wa Bajeti ya Wizara kwa nwaka wa fedha 2024/25 na utekelezaji wa majukumu ya barazi hilo katika Tawi la Wizara ya Maji.