Na Prisca Libaga Arusha
Zaidi ya wananchi 450 kutoka maeneo mbalimbali ya Mkoa wa Arusha wamepata huduma ya upasuaji wa Mtoto wa Jicho (cataract) bure, kupitia kampeni ya afya iliyoendeshwa na Madaktari Bingwa na Wabobezi kutoka nchini Hispania.
Huduma hiyo, iliyolenga kuwasaidia wananchi wa kipato cha chini, inafanyika katika Hospitali ya Wilaya ya Meru, na imepokelewa kwa furaha kubwa na jamii husika ambayo kwa muda mrefu imekuwa ikikumbwa na changamoto ya matatizo ya macho bila uwezo wa kupata matibabu stahiki.
Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mhe. Paul Christian Makonda, ametembelea hospitali hiyo kwa lengo la kuwapa pole wagonjwa waliokuwa wakipatiwa huduma, na kuwapongeza wahudumu wote waliofanikisha kampeni hiyo ya kibinadamu ambapo amewashukuru wataalam hao kwa moyo wa kujitoa kusaidia jamii, akisisitiza kuwa jitihada hizo zinaendana na maono ya serikali ya awamu ya sita ya kutoa huduma bora za afya kwa kila Mtanzania.
“Mafanikio haya ni matokeo ya mahusiano imara ambayo yamejengwa na Rais wetu, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kati ya Tanzania na mataifa mengine, jambo ambalo limefungua milango kwa mashirika na wadau mbalimbali kushirikiana nasi katika maendeleo ya sekta ya afya na Serikali itaendelea kushirikiana na wadau wote wanaogusa maisha ya wananchi kwa namna chanya kama ilivyofanyika hapa.” amesema Mhe. Makonda.
Hata hivyo, Wananchi waliopata huduma hiyo wameeleza jinsi walivyokuwa wakiteseka na matatizo ya macho, na sasa wanayafurahia matumaini mapya baada ya kuona tena huku wakitoa shukrani zao za dhati kwa Ras Dkt. Samia Suluhu Hassan Pamoja Mkuu wa Mkoa huo kwa upendo huo waliowanyesha.
Huduma hiyo ilianza kutolewa tarehe 13 Aprili na itahitimishwa 22 Aprili, 2025




