Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, amesema kuwa watu wenye ulemavu, wakiwemo wasanii wafupi, ni sehemu muhimu ya jamii na wanayo nafasi kubwa ya kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya taifa na kutoa elimu sahihi kuhusu mafanikio ya Serikali.
Akizungumza jijini Dar es Salaam wakati wa uteuzi wa timu ya wasanii wafupi wakiongozwa na Tausi Degela, Pimbi na Hamisi, Chalamila alisema hatua hiyo inalenga kuonesha kuwa kila kundi katika jamii lina mchango mkubwa katika kujenga nchi.
“Sisi ni wajukuu wa Samia, na tunatambua kuwa watu wenye ulemavu ni sehemu ya nguvu kazi ya taifa. Tunawapa nafasi ya kuelimisha jamii na kushiriki kwenye ajenda ya maendeleo,” amesema Chalamila.
Msanii Tausi Mdegela aliwataka watu wenye ulemavu kuachana na dhana ya utegemezi na kuanza kujishughulisha na shughuli za uzalishaji mali, akisisitiza kuwa ulemavu si kikwazo cha mafanikio.
“Tumewezeshwa kupitia mikopo na fursa nyingine. Tunapaswa kujiamini na kushiriki kikamilifu katika kuinua uchumi wetu binafsi na wa jamii,” amesema Tausi.
Kwa upande wake, msanii Pimbi alihamasisha watu wenye ulemavu kushiriki kikamilifu katika mchakato wa uchaguzi ujao, akisisitiza kuwa ushiriki wao ni wa muhimu katika maamuzi ya kitaifa.
“Ni wakati wetu wa kusimama na kuonekana. Tuna haki sawa kama Watanzania wengine, na tunapaswa kutumia sauti yetu ipasavyo,” amesema Pimbi.