Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Mlezi wa Chama cha Mawakili wa Serikali Mhe. Hamza S. Johari amekutana na kufanya mazungumzo na uongozi mpya wa Chama cha Mawakili wa Serikali( TPBA) kwa lengo la kuwapongeza viongozi waliochaguliwa, pamoja na kushuhudia zoezi la makabidhiano ya nyaraka muhimu za chama hicho.
Mwanasheria Mkuu wa Serikali amekutana na viongozi hao, Ofisini kwake Bungeni Jijini Dodoma, Jumatano tarehe 16 Aprili 2025.
Aidha, Mwanasheria Mkuu wa Serikali amewaahidi ushirikiano wa kutosha viongozi wapya wa Chama cha Mawakili wa Serikali huku akiwa na akielezea matumaini yake makubwa aliyonayo kwa viongozi hao katika kuendeleza yale yaliyoachwa na uongozi uliomaliza muda wao na kukipeleka chama hicho mbele zaidi.
*“Mimi kama mlezi wa chama hiki nawaahidi kuwapa ushiirkiano mkubwa na mtakapokuwa tayari na kujua nini mnataka kufanya katika ile STRATEGIC PLANNING mnakaribishwa wakati wowote kwa mlezi wenu ili niweze kuwapa hiyo support.”* Amesema Mwanasheria Mkuu wa Serikali
Aidha, Mhe. Johari ameshuhudia makabidhiano kati ya Uongozi uliomaliza muda wake na uongozi mpya wa Chama cha Mawakili wa Serikali.
Kwa upande wake, Rais wa Chama hicho aliyemaliza muda wake Bw. Amedeus Shayo amesema kuwa ana Imani kuwa, chama hicho kitaendelea kuwa imara kwakuwa kimepata viongozi makini wenye maono mapana huku akiwaahidi kuwapa ushirikiano katika kuendelea kukijenga chama hicho.
*“Nawaahidi kuwapa ushirikiano tuendelee kufanya kazi pamoja kwasababu kukijenga chama ni jukumu letu sote.”* Amesema Bw. Shayo
Naye Rais mpya wa Chama cha Mawakili wa Serikali Bw. Bavoo Junus amemshukuru Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Mlezi wa Chama hicho Mhe. Hamza S. Johari kwa maono yake ya kukiona chama hicho kuwa kinakuwa Chama kikubwa katika Ukanda huu wa Afrika Mashariki.
Vilevile Bw. Bavoo amesema uongozi wake umejipanga kutekeleza yale yote yaliyoanishwa kwenye mkakati wa Chama hicho kwa viwango na weledi na ili kukifanya chama kufikia malengo waliyojiwekea. Pia Rais huyo mpya amemshukuru Rais aliyemaliza muda wake kwa kujenga misingi imara ndani ya chama hicho.
*“Ninamshukuru Rais anayemaliza muda wake Bw. Shayo kwa kazi nzuri aliyoifanya katika kukijenga chama chetu na sisi kama viongozi wapya tutaendelea kushirikiana nae”.* Amesema Bw. Bavoo
Rais aliyemaliza muda wake Bw. Amedeus Shayo alifanya makabidhiano kwa kumkabidhi nyaraka mbalimbali za Chama cha Mawakili wa Serikali, Rais mpya wa Chama hicho Bw. Bavoo Junusi.