*Makalla apongeza hatua kubwa ya maendeleo iliyofanyika ya kuwa na halmashauri ya Mtama
LINDI: KATIBU wa Halmashauri Kuu (NEC), Itikadi Uenezi na Mafunzo wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), CPA Amos Makalla amesema kuwa Rais Samia Suluhu Hassan ameacha alama kwa Watanzania kwani amekuwa Rais wa vitendo kwa kuwagusa wananchi kupitia mambo mbalimbali ya maendeleo.
Makalla ameeleza hayo leo Aprili 14,2025 wakati akisalimia wananchi wa Jimbo la Mtama Wilaya ya Lindi Vijijini mkoani Lindi akihitimisha ziara yake katika Mkoa wa Lindi tayari kwa kuendelea katika Mkoa wa Mtwara ikiwa ni muendelezo wa ziara ya siku 10 katika mikoa hiyo miwili.
Makalla amesema watanzania wameguswa na Rais Samia kwenye mambo mbalimbali ya maendeleo ikiwemo umeme, maji, maji, elimu, afya, barabara, majengo ya utawala na sehemu nyingine nyingi kutokana na kuwa kiongozi wa vitendo na utekelezaji wa mambo ya maendeleo.
“Rais Samia Suluhu Hassan ni rais wa vitendo na sio wa maneno ameweka alama katika kila kitongoji, kijiji, kata, Wilaya, Kila jimbo na Tanzania nzima, wananchi wa Tanzania wameguswa na Rais Samia kwa kila kitu, wengine maji, elimu, umeme, afya, barabara, majengo ya utawala kila mahali Dk Samia amewagusa watanzani,” alisema Makalla.
Aidha, amepongeza hatua kubwa ya maendeleo iliyofanyika ya kuwa na halmashauri ya Mtama kwa sababu mambo mengi ya kushughulika na wananchi yapo katika halmashauri, hivyo wataweza kuwahudumia wananchi wao kwa wakati.
Pia Makalla amewataka wananchi waendelee kuamini serikali hususani katika suala la stakabadhi ghalani kwani ni msaada kwa wakulima kwa kuwasaidia kufanya mapinduzi katika mazao ya Korosho, mbaazi na ufuta na kuahidi kuwa watawaletea ilani nzuri itakayoendelea jushughulika na changamoto za watanzania.
Katika hatua nyingine aliwataka wana CCM wa Mtama wampokee Katibu wa Wilaya ya Lindi Vijijini kutoka Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) aliyehamia CCM, Hamis Mtanda na wenzake wawape ushirikiano kwani wanaongeza kura za chama hicho.