Msoga, Chalinze — Ilikuwa ni siku ya kihistoria na ya kipekee kabisa kijijini Msoga, Alhamisi Aprili 10, 2025, wakati Rais mstaafu Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete alipobeba Mwenge wa Uhuru mbele ya mamia ya wananchi waliomiminika kushuhudia tukio hilo la kihistoria.
Mwenge wa Uhuru ulipowasili rasmi mkoani Pwani, kijiji cha Msoga — hususan nyumbani kwa Rais huyo mstaafu — kiligeuka jukwaa la furaha, vigelegele na nyimbo za kizalendo. Kikwete, akiwa mwenye bashasha na msisimko, alibeba mwenge huo kwa mikono miwili huku akiushikilia kwa uhodari unaoashiria uzalendo na kumbukumbu ya safari ya ukombozi wa taifa.
Akizungumza kwa bashasha na msisimko wa aina yake, Rais Mstaafu Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete alisema:
“Ni furaha na heshima kubwa kushiriki na wananchi wenzangu wa Msoga, kupokea Mwenge wa Uhuru kijijini kwetu. Hili ni tukio la kihistoria na la kujivunia sana. Mwenge huu umebeba ujumbe wa matumaini, mshikamano na maendeleo.”
Akaongeza kwa tabasamu:
“Hakika elimu haina mwisho. Leo nimejifunza jambo muhimu sana—niliona vijana wa Kikosi cha Wakimbiza Mwenge wakikagua ubora wa majengo ya Sekondari mpya ya Amali inayojengwa hapa kwetu Msoga. Kilichonifurahisha zaidi ni namna walivyotumia vifaa na teknolojia ya kisasa kabisa kufanya ukaguzi wao. Hawakubahatisha hata kidogo. Kila kitu kilikuwa kwa viwango na taratibu!”
Rais mstaafu hakusita kutoa pongezi kwa serikali ya sasa:
“Natoa pongezi nyingi kwa Rais Samia Suluhu Hassan kwa kazi nzuri na yenye tija anayoendelea kuifanya. Kasi yake ya kuimarisha elimu, afya, miundombinu na maendeleo ya kijiji kama Msoga ni ya kuigwa. Hili ni Taifa letu sote—na linapokua, nasi tunakua pamoja nalo.”
Alimaliza kwa kuhimiza vijana wa Msoga na Tanzania kwa ujumla kuendelea kuthamini Mwenge wa Uhuru kama ishara ya umoja, uzalendo na maendeleo yanayogusa maisha ya kila Mtanzania.