Simba SC imefanikiwa kutinga hatua ya nusu fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika baada ya kupata ushindi wa penalti 4 -1 dhidi ya Al Masry ya Misri katika mchezo uliochezwa leo April 9, 2025 katika Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.
Hatua ya mikwaju ya penati imekuja baada ya Simba SC kushinda 2-1 ndani ya dakika 90 mabao ya winga Mkongo, Elie Mpanzu dakika ya 22 na mshambuliaji Mganda Steven Dese Mukwala dakika ya 32.
Ushindi huo ulifanya matokeo ya jumla kuwa sare ya 2-2 kufuatia Al Masry kushinda 2-0 katika mchezo wa kwanza uliopigwa April 2 mjini Ismailia.
Kipa wa Simba SC Mguinea, Moussa Camara ameibuka shujaa kwa kuokoa mikwaju miwili ya penalti za viungo Mohamed Gaber Tawfik Hussein na Mahmoud Hamada Awad, huku Fakhreddine Ben Youssef akimfunga bao pekee.
Waliofunga penalti kwa Simba SC ni Ahoua, Mukwala, kiungo mshambuliaji Kibu Denis Prosper, Beki Shomari Salum Kapombe.
Simba SC sasa itakutana na mshindi wa jumla kati ya wenyeji Zamalek na Stellenbosch ya Afrika Kusini zinazorudiana usiku wa leo Uwanja wa Cairo International baada ya timu hizo kutoka suruhu kwenye mchezo wa kwanza April 2, katika Uwanja wa DHL Cape Town.