Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya Chama Cha Waajiri Tanzania (ATE) Bi. Imelda Lutebinga (kushoto) akijadiliana jambo na wanafunzi wa Chuo Kikuu Mzumbe, Ndaki ya Dar es Salaam, Kituo cha Tegeta wakati akitoa mafunzo ya kuwajengea uwezo yaliofanyika April 4, 2025, Dar es Salaam.

Mfanyakazi wa Chama Cha Waajiri Tanzania (wa kwanza kulia) akiwa na Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya ATE Bi. Imelda Lutebinga wakifatilia jambo katika mafunzo ya kuwajengea uwezo  wanafunzi wa chuo kikuu mzumbe ndaki ya Dar es Salaam.

Naibu Rasi wa Chuo Kikuu Mzumbe Ndaki ya Dar es Salaam, Prof. Omary Swalehe akizungumza jambo na Balozi wa Norway Nchini, Mhe. Tone Tinnes.

Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya Chama Cha Waajiri Tanzania (ATE) Bi. Imelda Lutebinga akimkabidhi zawadi mwanafunzi wa chuo Kikuu Mzumbe, ndaki ya Dar es  Salaam.

Wanafunzi wa Chuo Kikuu Mzumbe, Kituo cha Tegeta wakiwa katika picha ya pamoja na viongozi wa Chuo hicho, Ubalozi wa Norway nchini Tanzania, Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya Chama cha Waajiri Tanzania (ATE) pamoja na Taasisi za kibiashara nchini Norway (NHO)

………….

NA NOEL RUKANUGA, DAR ES SALAAM

Chama cha Waajiri Tanzania (ATE) wametoa mafunzo ya usawa katika uongozi na biashara kwa wanafunzi wa Chuo Kikuu Mzumbe, Ndaki ya Dar es Salaam, kituo cha Tegeta ili kuwasaidia kujimudu katika nyanja mbalimbali hasa katika nafasi ya uongozi unaozingatia uwasa wa kijinsia mahali pa kazi.

Akizungumza leo April 4, 2025 jijini Dar es Salaam wakati akitoa mafunzo kwa wanafunzi wa Chuo Kikuu Mzumbe, Ndaki ya Dar es Salaam, Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya Chama cha Waajiri Tanzania (ATE) Bi. Imelda Lutebinga, amesema kuwa ni muhimu kutoa elimu kwa wanafunzi ikiwa ni sehemu ya kupanda mbegu itakayosaidia Taifa.

Lutebinga, amesema kuwa mafunzo ya usawa katika uongozi na biashara ni rafiki kwa wanafunzi wa vyuo vikuu kwani yamegusa nyanya tofauti ikiwemo namna bora ya kuanzisha biashara pamoja na kutoa fursa ya kupata nyenzo itakayowasaidia baada ya kumaliza masomo yao.

“Nilikuwa mwanafunzi wa Chuo Kikuu Mzumbe miaka 15 iliyopita na sasa nimepata fursa ya kushiriki katika nafasi ya maamuzi katika maeneo tofauti ili kulisaidia Taifa katika kuendeleza dira” amesema Lutebinga.

Lutebinga amesema kuwa ATE imekuwa na utamaduni wa kuendesha programu mbalimbali nchini ikiwemo kuwajengea uwezo wanawake kulingana na uhitaji hasa katika nafasi ya uongozi.

Amefafanua kuwa mpaka sasa wamefanikiwa kutoa elimu kwa wahitimu zaidi ya 600 katika Serikali ya Tanzania Bara na mapinduzi ya Zanzibar.

Amesema kuwa wanaendelea kutoa elimu ya mafunzo mbalimbali katika jamii ikiwemo kujiamini, kujieleza kwa ufasaha ili kuhakikisha wanawake wanakuwa na uwezo mkubwa wa kuongoza katika nafasi yoyote ya uongozi.

Katika mafunzo hayo kulikuwa na watoa mada kutoka Taasisi mbalimbali ikiwemo Taasisi za biashara kutoka nchini Norway, Chuo Kikuu Mzumbe pamoja na Tanzania Startup Association ambapo wamesisitiza umuhimu wa wanafunzi kuwa na subira pamoja na kutengeneza mahusiano mazuri na wadau ili kufikia fursa kwa haraka baada ya kumaliza masomo.

Kwa upande wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Mzumbe, Kituo Cha Tegeta wametoa shukrani kwa kupata mafunzo, kwani yamewasaidia kujifunza mbinu bora za kuanzisha na kuendesha biashara pamoja na uongozi ambazo zitawasaidia kuwa viongozi bora katika jamii na maeneo ya kazi.