Lori aina ya Fuso lenye namba T704 DCD lililokwama jana saa 12;00 jioni katika daraja la barabara ya Fullo -Nyambiti ambalo lilikuwa likiendeshwa na dereva Deo Mathias Kachelwo wa Sumve, lori hilo lilisababisha adha kwa magari na Wasafiri wanaotumia barabara hiyo, hii ni kutokana na ubovu wa barabara unaosababishwa na mvua zinazoendelea kunyesha.
……………………………………………………………………………………………………………..
Mkuu wa Wilaya ya Misungwi, Juma Sweda aagiza Wakala wa barabara Mkoani Mwanza, (TANROADS) kuhakikisha wanafanya matengenezo ya dharula katika barabara ya Fullo – Nyabiti iliyopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Misungwi Mkoani Mwanza.
Ametoa agizo hilo mapema leo baada ya kushuhudia na kuona hali halisi ya ajali iliyotokea ya Lori aina ya Fusso lenye namba T 704 DCD la Sumve lililokwama usiku wa tarehe 27 mwezi huu katika daraja la Bujingwa- Kanyelele na kusababisha adha na kero kwa Wananchi na magari yanayopita katika barabara hiyo yakitokea Jiji la Mwanza kuelekea maeneo ya Sumve na Nyabiti Wilaya ya Kwimba.
“ Naitaka Wakala ya barabara Mkoa wafike na kuona namna miundombinu ya barabara ilivyo kwa sasa, pamoja na madaraja yameanza kubomoka kutokana na mvua hii inayoendelea na wachukue hatua kwa kufanya matengenezo haraka ili kunusuru na kuondokana na kero ya usafiri kwa Wananchi, abiria na magari ya mizigo”, alisisitiza Mkuu wa Wilaya Sweda.
Amewataka Wananchi Wilayani Misungwi kuchukua tahadhari hususani nyakati hizi za mvua wanapotumia barabara na kuwa wangalifu kwenye madaraja ya barabara hizo za vijijini ili kuepuka madhara na uharibifu zaidi wa miundombinu pamoja na kuwa watulivu na kuendelea kuchapa kazi kwa ajili ya kuleta maendeleo na kujenga uchumi wao na taifa kwa ujumla.
Akizungumza kwa njia ya simu Mwakilishi wa Meneja wa Wakala wa barabara (TANROADS) Mkoa wa Mwanza Mhandisi Joseph Pius Mwami amesema kwamba tayari Wataalam wa uhandisi wameshafika katika maeneo ya barabara hiyo ya Fullo – Nyabiti na wamejiridhisha na kuona miundombinu ya barabara na madaraja yaliyoharibika katika barabara hiyo kutokana na mvua zinazoendelea na hatua za matengenezo zitaanza hivi karibuni.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Misungwi, Kisena Mabuba (kulia) wakiangalia na kushuhuhudia namna Lori lililokuwa limebeba mizigo kutoka Mwanza baada ya kukwama katika daraja la Bujingwa -Kanyelele lilolopo kwenye barabara ya Fullo – Nyambiti inayopita Wilayani Misungwi, (katikati) ni Mkuu wa Wilaya ya Misungwi Juma Sweda akiwa pamoja na baadhi ya wajumbe wa Kamati ya ulinzi na usalama ya Wilaya akihakikisha usalama wa Wananchi na mali zao upo vizuri.
Mhandisi Joseph Pius Mwami amesema kwamba Wakala imeshachukua hatua muda kwa kutoa Zabuni ya matengenezo na Mkandarasi tayari ameshapatikana kwa ajili ya matengenezo ya barabara hiyo ya Fullo – Nyambiti yenye urefu wa kilomita 48, zitokazo meneo ya Bujingwa Wilayani Misungwi hadi Nyambiti Wilayani Kwimba.
Ameongeza kwamba tayari hatua za manunuzi kwa ajili ya matengenezo ya barabara hiyo zimeshafanyika na zitakapokamilika ujenzi utaanza mara moja na Wakala itahakikisha mataengenezo ya barabara hiyo yanafanyika kwa kiwango na ubora unaokubalika kwa mujibu wa taratibu na sheria.
Ametoa Wito kwa Wananchi kuwa wavumilivu hususani wakati huu wa mvua na kueleza kuwa Wakala itasimamia kikamilifu matengenezo hayo ili yaweze kukamilika kwa wakati na kurahisisha shughuli za usafiri na usafirishaji wa mali na mizigo katika maeneo husika na kuwaomba kutoa ushirikiano wakati wote wa ujenzi.