Tarime, Mara – Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) Mkoa wa Mara, Mary Daniel, amewataka vijana wa mkoa huo kuacha kujihusisha na vitendo vinavyochafua taswira ya Umoja huo, badala yake wawe mfano wa kuigwa kwa kutetea na kusaidia jamii wanapohitajika.
Akizungumza na vijana wa Wilaya ya Tarime wakati wa hitimisho la ziara yake ya kusikiliza na kutatua kero mbalimbali, Mary aliwasisitiza vijana kuheshimu sheria na kuzingatia maadili katika utendaji wao wa kila siku.
“Mnapovaa sare za Umoja huu, acheni kujiona kuwa mko juu ya wengine. Fanyeni kazi zenu kwa kufuata sheria, mjiheshimu na mheshimu jamii mnayoihudumia. Hii itawajengea heshima na kuwa kielelezo cha uadilifu,” alisema Mary.
Aidha, katika hatua nyingine, aliwahimiza vijana kuchangamkia fursa za mikopo ya vikundi zinazotolewa na Serikali, akiwataka kuunda vikundi vyenye malengo thabiti ili waweze kupata msaada na kunufaika na mikopo hiyo kwa maendeleo yao.
Mary alisisitiza kuwa vijana wanapaswa kutumia rasilimali na fursa zilizopo ili kujikwamua kiuchumi na kuwa mstari wa mbele katika kuchochea maendeleo ya jamii yao.