Kamishna wa Uhifadhi wa Mamlaka ya hifadhi wa Ngorogoro (NCAA) Dkt Freddy Manongi akiongea na watumishi wa Mamlaka hiyo wakati kikao cha kusikiliza maoni, kero na ushauri katika kuboresha utendaji kazi.
Naibu kamishna wa NCAA anayesimamia huduma za Shirika Bw. Asangye Bangu akijibu hoja mbalimbali za watumishi wakati wa kikao cha pamoja na watumishi hao.
Viongozi wa Kimila wa kabila la Kimasai (Laigwanan) wakimsikiliza kamishna wa Uhifadhi wa NCAA Dkt Freddy Manongi katika kikao cha pamoja kujadiliana mambo mbalimbali kuhusu uhifadhi.
……………………………………………………………………………………………………………..
Kamishna wa Uhifadhi wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro Dkt Freddy Manongi amewapongeza watumishi wa Mamlaka hiyo kwa kufanya kazi kwa bidii, uzalendo na kujituma katika kutimiza malengo ya Mamlaka hiyo.
Dkt Manongi ametoa pongezi hizo wakati akizungumza na watumishi wa Mamlaka hiyo ikiwa ni utaratibu aliojiwekea wa kukutana na watumishi na kusikiliza kero, maoni, ushauri na malalamiko yanayohusu utendaji kazi wa watumishi na namna ya kuendelea kuboresha mazingira ya utendaji kazi.
Kamishna Manongi amebainisha kuwa jitihada za watumishi wa NCAA zimesaidia ongezeko la mapato ya shirika kutoka makusanyo ya shilingi bilioni 60 mwaka 2014/2015 hadi kufikia kiasi cha shilingi Bilioni 143 katika mwaka wa fedha 2018/2019.
“Ushirikiano, kujituma na jitihada katika kazi umetusaidia kutimiza malengo tuliyopewa na kupelekea ongezeko la mapato kutoka Bilioni 60 mwaka 2015 hadi Bilioni 143 mwaka 2018/2019 na tunaamini kama tutaendelea na moyo huu wa kufanya kazi kwa moyo tutaisaidia Serikali yetu kuongeza mapato zaidi kwa miaka ijayo” ameongeza Dkt Manongi.
Kwa upande wake Naibu Mhifadhi wa Mamlaka hiyo anayesimamia huduma za Shirika Bw. Asangye Bangu amewahakikishia watumishi hao kuwa NCAA itaendelea kuweka utaratibu wa kuhakikisha kuwa watumishi wanaendelea kupata mafunzo ya muda mfupi na mrefu ili kuwaongezea uwezo na tija katik utendaji kazi wao ili kutimiza malengo makuu matatu yay a mamlaka ambayo ni uhifadhi, utalii na maendeleo ya jamii.
Katika kuhakikisha NCAA inaboresha huduma kwa wadau wake Mamlaka hiyo inatarajia kuanzisha kituo cha huduma kwa wateja (Customer Call Centre) Jijini Arusha hivi karibuni ili kusaidia wadau mbalimbali katika upatikanaji wa huduma popote wanapokuwa bila kulazimika kufika ofisini.
Meneja Rasilimaliwatu wa Mamlaka hiyo Bw. Samson Ntunga amewaasa watumishi wa NCAA kuendelea kufanya kazi kwa uadilifu, uaminifu, uvumilivu, upendo, kuepuka migogoro na kuhakikisha kuwa wanazingatia maadili na misingi ya utendaji kazi katika utumishi wa Umma.
Katika hatua nyingine Uongozi na watumishi wa NCAA walitumia fursa ya kikao hicho kukutana na viongozi wa jamii ya Kimasai (Laigwanan) ambao ni wenyeji wanaoshi katika hifadhi ya Ngorongoro ikiwa ni sehemu ya mikutano endelevu ya kujadili mahusiano ya utendaji kazi na jamii hiyo, changamoto na mbinu mbalimbali katika kuendeleza kazi za uhifadhi kama sehemu ya wadau muhimu katika hifadhi hiyo.