…………….
Na Mwandishi Wetu – Njombe
Wananchi Wilayani Makete Mkoani Njombe, wametakiwa kutunza mazingira pamoja na vyanzo vya maji kwa kupanda Miti rafiki kwenye maeneo yao ili iweze kuwasaidia katika Uhifadhi wa rasilimali za Misitu kwa kizazi hiki na kijacho
Wito huo imetolewa leo Machi 15, 2025 Mkoani Njombe na Bw. Agustino Ngajilo, Afisa Tarafa ya Lupalilio, katika siku ya pili ya upandaji wa miti kitaifa katika Halmashauri za Wilaya za Mkoa wa Njombe ambapo amesema hatua hiyo itasaidia katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi na uhifadhi ya rasilimali zilizopo
“Niwasihi wananchi wenzangu kuacha tabia ya kuchoma moto hivyo misitu kwakuwa hupekeka uharibufu mkubwa wa mazingira na kupelekea hasara kwa wananchi na serikali kwa ujumla” Amesema Ngajilo
Naye, Afisa Misitu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii Bw. Emmanuel Msoffe, amewapongeza wananchi wa Wilaya ya Makete kwa kutunza mazingira kwa kupanda miti kwa wingi, huku akiwataka kuitunza miti ya asili kwa ajili ya uhumilivu wa mazingira.
“Nachukua fursa hii kuwapongeza wananchi kwa kuamua kuacha kazi zenu na kuungana nasi katika zoezi hili la Upandaji Miti katika Wilaya yenu, sisi kama wawakilishi wa Wizara tutaendelea kuwa na nyinyi kupitia kampeni hii ya utunzaji Miti na uhifadhi wa Misitu kwa kuwa ndio maono ya kiongozi wetu wa nchi Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan katika Uhifadhi wa Misitu hapa nchini”Amesema Bw. Msoffe
Kwa Upande wake, Afisa Mazingira wa Halmashauri ya Wilaya ya Makete, Bi. Upendo Mgaya, ametoa rai kwa wananchi wa Wilaya hiyo, kuitunza miti hiyo na kuacha kupanda miti isiyo rafiki na Mazingira kwenye vyanzo vya maji sambamba na maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya kilimo
Jumla ya Miche ya parachichi 100 na miti ya mapambo 150 jumla ikiwa miti 250 imepandwa katika shule hiyo kupitia zoezi hilo likihudhuriwa na wataalamu kutoka Wizara ya Mali Asili na Utalii, Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Njombe pamoja na wataalamu mbalimbali kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Makete.
Itakumbukwa Machi 21, kila mwaka Tanzania huungana na mataifa mengine duniani kuadhimisha Siku ya Misitu Duniani na siku ya Upandaji Miti kitaifa ambapo kwa mwaka huu maadhimisho hayo kitaifa yanafanyika Mkoani Njombe