Farida Mangube, Morogoro
Mamia ya wafanyabiashara wa Halmashauri ya Mlimba, Wilaya ya Kilombero, wamejitokeza kwa wingi kushiriki semina ya elimu ya kodi iliyoandaliwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) mkoa wa Morogoro, yenye lengo la kuwaelimisha na kuwakumbusha umuhimu wa kulipa kodi.
Akizungumza katika semina hiyo, Meneja wa TRA Mkoa wa Morogoro, Bw. Sylver Rutagwelera, alisema kuwa semina hiyo ni sehemu ya utaratibu wa TRA wa kukutana na walipakodi kila Alhamisi ili kuwasikiliza, kutatua changamoto zao, na kupokea maoni yao kwa ajili ya kuboresha huduma.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Kilombero, Mhe. Dunstan Kyobya, ameiomba TRA kusogeza huduma zake karibu na wafanyabiashara wa Mlimba, akieleza kuwa eneo hilo linaendelea kukua kibiashara lakini linakabiliwa na changamoto ya umbali wa zaidi ya kilomita 100 kufuata huduma za TRA wilayani Kilombero.
“Hii ni changamoto kubwa kwa wafanyabiashara wetu. Ni muhimu kwa TRA kufungua ofisi hapa Mlimba ili kuwasaidia kulipa kodi kwa wakati na kuimarisha ukusanyaji wa mapato ya serikali,” alisema Mhe. Kyobya.
Katika semina hiyo, wafanyabiashara walipata fursa ya kuelewa wajibu wao wa kulipa kodi na kushiriki majadiliano ya wazi kuhusu changamoto wanazokutana nazo. Mwisho wa semina, washiriki walieleza kuridhishwa na mafunzo waliyopata na kuahidi kushirikiana na TRA katika kutekeleza wajibu wao wa kikodi.