Wateja wa MSD kutoka mikoa ya Mbeya, Songwe, Rukwa, na halmashauri ya Makete Wahimizwa kutumia vyanzo vingine vya mapato kununua bidhaa za afya kutoka Bohari ya Dawa (MSD).
Aidha wametakiwa kulipa au kupunguza madeni yao wanayodaiwa na MSD ili kuipa nguvu ya kiuchumi katika mzunguko wa ugavi wa bidhaa za afya, badala ya kurundika madeni yao.
Rai hiyo imetolea na Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Dkt. Elizabeth Nyema kwa niaba ya Katibu Tawala wa Mkoa wa huo, wakati wa ufunguzi wa kikao cha Wateja na Wadau wa MSD Kanda ya Mbeya 2025, kilichofanyika katika ukumbi wa hoteli ya Tughimbe, jijini Mbeya.
“Kama wasimamizi wa huduma za afya kwenye maeneo yenu, mnao wajibu na jukumu kubwa la kusimamia vituo vyenu, kuhakikisha vinakusanya mapato ya kutosha, yatokanayo na uchagiaji wa huduma ili viweze kununua bidhaa na kulipa madeni yao MSD.” Alisema Dkt. Nyema
Ameongeza kuwa, kutolipa madeni ya MSD ni kudumaza huduma, kwani madeni hayo yanaathiri mnyororo wa ugavi wa bidhaa za afya, na vituo vitashindwa kuhudumiwa ipasavyo na MSD itakosa fedha kuendeleza mzunguko wa upatikanaji wa bidhaa za afya.
Dkt. Nyema ameipongeza MSD kwa kuandaa vikao vya Wadau, ambavyo vinawaleta pamoja wataalamu wa Afya na kujadili namna nzuri ya kutatua changamoto zinazoukabili mnyororo wa ugavi na kuzitafutia utatuzi.
Dkt. Nyema amesisitiza kwamba afya ni nguzo kubwa ya maendeleo kwa mwananchi mmoja mmoja na taifa kwa ujumla, hivyo uwepo wa vikao hivyo ni chachu ya maboresho ya huduma za afya nchini.
Awali akitoa salaam za utangulizi, Kaimu Meneja wa MSD Kanda ya Mbeya Bw. Petro Mdegela amesema Kanda hiyo inahudumia vituo vya kutolea huduma za afya takribani 960, ambapo mkoa wa Mbeya una vituo 416, Songwe 248, Rukwa 236 na Makete vituo 60.
Mdegela ameongeza kwamba MSD Kanda ya Mbeya kama kanda nyingine za MSD husambaza bidhaa za afya hadi mlangoni kwa mteja, mara 6 kwa mwaka, hatua ambayo imesaidia kwa kiasi kikubwa, kuondoa upungufu wa bidhaa za afya nchini.
Ameongeza kwamba MSD inaendelea kuhakikisha madai yote ya nyuma ya vifaa tiba ya Wateja, yanafanyiwa kazi na kuwasilishwa kwao haraka iwezekanavyo, kwani menejimenti ya MSD imekwisha fanyia kazi eneo hilo.
Mdegela amewaomba wateja na Wadau hao wanaohudumiwa na Kanda hiyo, kuendelea kushirikiana na MSD ili kwa pamoja waweze kuboresha na kuimarisha mnyororo wa ugavi wa bidhaa za afya nchini.
Akifunga kikao hicho Mganga Mkuu wa Mkoa wa Songwe, Dkt. Boniface Kasululu amesema kikao hicho kimekuwa na mafanikio na tija kwa mikoa yote inayohudumiwa na Kanda hiyo, kwani pande zote mbili zimejadiliana kwa uwazi, kupata maelezo na maoni mbalimbali kwa ajili ya kuboresha upatikanaji wa bidhaa za afya.
Dkt. Kasululu amewataka Wadau hao kuhakikisha wanafanyia kazi yale yote yaliyoibuliwa kwenye kikao hicho, mathalani uwasilishaji maombi ya bidhaa kwa wakati, ulipaji wa madeni, mashirikiano, matengenezo ya vifaa tiba, vipuli vya mashine mbalimbali zinazo sambazwa na MSD, matengenezo ya wakati kwa Vifaa tiba.nk.
Na nwisho Dkt. Kasululu ameipongeza MSD kwa maboresho ya huduma na upatikanaji wa bidhaa za afya, kwani hivi sasa upatikanaji huo umepanda maradufu, ukilinganisha na kipindi cha nyuma ambapo malalamiko yalikuwa mengi.