Na Mwamvua Mwinyi,Pwani
Machi 11,2025
Maandalizi ya uwanja utakaotumika kuwasha Mwenge wa Uhuru
Na Mwamvua Mwinyi,Pwani
Machi 11,2025
Maandalizi ya uwanja utakaotumika kuwasha Mwenge wa Uhuru katika viwanja vya Shirika la Elimu Kibaha, mkoani Pwani, april 2 mwaka huu yafikia asilimia 70.
Hayo yamebainika wakati Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Ridhiwani Kikwete, alikwenda kukagua maandalizi ya uwanja huo.
Baada ya ukaguzi huo, Waziri Kikwete alieleza kuridhishwa na maendeleo ya maandalizi hayo huku akihimiza kuongeza kasi ili kuhakikisha kazi inakamilika kwa wakati uliopangwa.
Alisisitiza umuhimu wa kufundisha watoto kuhusu uzalendo, akisema kuwa inawasaidia kuelewa kwa undani maendeleo yaliyopatikana kupitia usimamizi wa viongozi waliotangulia.
Aidha, Waziri Kikwete alibainisha kuwa ujumbe wa Mwenge wa Uhuru 2025 unalenga kuhamasisha wananchi kutumia haki yao ya msingi ya kupiga kura katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025.
Ujumbe huo pia utahimiza mapambano dhidi ya rushwa, utunzaji wa afya, na kutoa kipaumbele kwa kilimo, huku ukisisitiza mshikamano wa kitaifa.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Abubakar Kunenge, alisema maandalizi ya uwanja huo yamefikia asilimia 70, na wanatarajia ifikapo Machi 20, 2025, kazi hiyo itakuwa imekamilika, ikiwa ni pamoja na kuanza kwa uunganishaji wa miundombinu ya umeme.
“Kila kitu kipo vizuri, kuanzia ulinzi hadi maandalizi ya uzinduzi, Tutawasha Mwenge wa Uhuru hapa Pwani na kuanza kuukimbiza.
Ninawaomba wananchi tujitokeze kwa wingi, tuitendee haki heshima tuliyopewa,” alisema Kunenge.
Mwenge wa Uhuru unatarajiwa kuwashwa rasmi tarehe 2 Aprili 2025 katika viwanja vya Shirika la Elimu Kibaha, mkoani Pwani.