Na. Elimu ya Afya kwa Umma.
Timu ya Wataalamu wa Afya kutoka Programu ya Mafunzo ya Epidemiolojia (TFELTP) imejivunia na hatua za Serikali kwa kuimarisha suala la Ufuatiliaji wa Magonjwa ya mlipuko Wilayani Biharamulo hasa katika mapambano ya ugonjwa wa Marburg.
Akizungumza Wilayani Biharamulo, Msimamizi wa Timu ya Wataalamu Programu hiyo ya Mafunzo ya Epidemiolojia (TFELTP) Bw. Solomon Werema kutoka Wizara ya Afya, Idara ya Kinga, Sehemu ya Epidemiolojia amesema timu hiyo ya wataaamu wanafunzi wanaosomea masomo ya Epidemiolojia imesaidia katika ufuatiliaji wa tetesi kwa magonjwa ya mlipuko .
“Jambo la kujivunia ni kuwa imesaidia ufuatiliaji wa Wagonjwa wenye dalili zinazofafana na ugonjwa wa Marburg Wilayani Biharamulo(Active Case Search) na timu imeweza kutembelea vituo vya Afya na kuhakikisha taarifa zinaripotiwa kwa wakati”amesema.
Emmanuel Costantine ni Mwanafunzi kutoka Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili masomo ya Epidemiolojia amesema lengo la kuja Wilaya ya Biharamulo ni kufuatilia Wagonjwa wenye dalili zinazofanana na ugonjwa wa Marburg tangu tarehe 3, Machi, 2025 na kuhitimisha tarehe 10, Machi, 2025 na kufanikiwa kufikia vituo vya kutolea huduma za afya 13.
“Tumefanikiwa kufikia vituo vya kutolea huduma za afya 13 na kuwajengea uwezo watoa huduma kwenye vituo vya huduma za afya na Watoa Huduma za Afya Ngazi ya Jamii katika kutambua dalili mapema za magonjwa ya mlipuko na kuweza kuhudhuria vituo vya kutolea huduma za afya ”amesema .
Tarehe 10, Machi, 2025 Madaktari kutoka Timu Wataalamu wa Afya wa Programu ya Mafunzo ya Epidemiolojia (TFELTP) Dkt. Muzzna Ujudi, Dkt. Bahati Libenenga, Dkt. Monga Nyalla na Dkt. Enock Mwabalasa wametembelea katika Kituo cha Afya cha Bisibo Wilayani Biharamulo Mkoani Kagera kisha kutembelea Biharamulo Council Designated Hospital.
Ikumbukwe kuwa unaweza kujikinga na ugonjwa wa Marburg kwa;
✅Kuepuka kugusana na mtu mwingine mfano kusalimiana kwa kushikana mikono,kukumbatiana au kubusiana.
✅Kuepuka kugusa majimaji ya mwili wa mtu mwenye dalili za ugonjwa wa Marburg.
✅Kuepuka kugusa vitu kama vile vyombo, matandiko, magodoro vilivyotumiwa na mtu mwenye dalili za ugonjwa wa Marburg.
✅Kuepuka kuchangia vitu chenye ncha kali na mtu mwenye Maambukizi .
✅Kunawa mikono kwa maji tiririka na sabuni mara kwa mara