Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Mahmoud Thabit Kombo (Mb.) amepongeza maboresho makubwa yanayofanywa katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Arusha (AICC).
Balozi Kombo ametoa pongezi hizo alipotembelea Kituo hicho hivi karibuni na kujionea maboresho yanayofanyika kituoni hapo ikiwemo ya Kumbi za Mikutano, mazingira na miundombinu mbalimbali.
Balozi Kombo ambaye alipokelewa kituoni hapo na Mkurugenzi wa Kituo hicho, Bi. Christin Mwakatobe amesema kuwa, maboresho hayo ambayo yanafanyika ili kukidhi mahitaji makubwa ya kumbi za mikutano hususan ile ya kikanda na kimataifa yanaendana na kasi ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kutangaza na kukuza sekta ya utalii ya hapa nchini kupitia mikutano.