Na Mwandishi wetu, Mirerani
KAMPUNI ya uchimbaji madini ya Chusa Mining LTD, imejitolea kujenga wodi mpya ya wanawake, watoto na ofisi ya madaktari wa kituo cha afya Mirerani, Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara, ili kizidi kukiboresha na kutoa huduma zaidi kwa jamii.
Kituo cha afya Mirerani kina changamoto ya upungufu wa wodi ya wanawake na watoto na kusababisha msongamano kwa wagonjwa wanapolazwa kwani kinahudumia baadhi ya watu wa wilaya za Simanjiro mkoani Manyara na Arumeru mkoani Kilimanjaro.
Mdau wa maendeleo wa Simanjiro, Sporah Mwakipesile kupitia kampuni ya Chusa Mining LTD, ametoa ahadi hiyo kwenye maadhimisho ya siku ya wanawake duniani iliyofanyika mji mdogo wa Mirerani.
Sporah amesema ameamua kufanya hivyo, baada ya kutembelea kituo cha afya Mirerani na kusikiliza changamoto za upungufu wa wodi ya wanawake, watoto na ofisi ya madaktari.
Amesema kwa sababu familia yake inafanya shughuli za uchimbaji madini ya Tanzanite mji mdogo wa Mirerani ni vyema kuchangia huduma za afya ili ziboreshwe zaidi.
Hata hivyo, ametembelea shule ya msingi Songambele ya watoto wenye uhitaji maalum na kuchangia vitanda 60, magodoro 120 na viti mwendo 10 kwa watoto wenye ulemavu.
“Ili kuniunga mkono katika sadaka hii tuchangieni kwa pamoja mashuka ila hayo mwingine kampuni yetu ya Chusa Mining LTD itachangia katika kuboresha huduma hizo na ujenzi wa wodi unaanza jumatatu ijayo,” amesema Sporah.
Mganga mkuu wa Halmashauri ya wilaya ya Simanjiro Dkt Lengai Edward ameishukuru kampuni ya Chusa Mining LTD, kwa kuiunga mkono serikali na kuboresha huduma za afya katika kituo cha afya Mirerani.
Dkt Edward amesema kituo cha afya Mirerani kina changamoto ya upungufu wa wodi ya wanawake na watoto kutokana na msongamano wa wagonjwa kwani kinahudumia baadhi ya watu wa wilaya za Simanjiro mkoani Manyara na Arumeru mkoani Arusha.
“Kwa niaba ya mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Simanjiro tunawashukuru kampuni ya Chusa Mining LTD, kwa kufanya jambo hili jema,” amesema Dkt Edward.
Mkurugenzi wa shule ya awali na msingi Glisten ya mji mdogo wa Mirerani, Justin Nyari ameunga mkono hafla hiyo kwa kutoa Sh1 milioni ili kununua mashuka ya watoto wa mahitaji maalum shule ya msingi Songambele.
Nyari amesema anaiunga mkono serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan kwa namna inayofanikisha maendeleo ya sekta mbalimbali kwa jamii.
Ofisa maendeleo ya jamii mji mdogo wa Mirerani, Floriana Mcharo amesema siku hiyo ya wanawake duniani imekuwa na baraka kwa jamii kutokana na hatua zilizofanywa.
Mkazi wa mji mdogo wa Mirerani, Peris Mwanyika ambaye amechangia Sh1 milioni amesema ni vyema kuchangia jamii ili huduma kwa watu zizidi kuboreshwa.
Mkazi mwingine wa mji mdogo wa Mirerani, Kilei Juma ambaye amechangia Sh300,000 ameipongeza kampuni ya Chusa Mining LTD kwa kufanya jambo kubwa la maendeleo.
