Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akizindua mradi wa maji wa Same-Mwanga-Korogwe kwenye hafla iliyofanyika Mwanga mkoani Kilimanjaro tarehe 09 Machi, 2025.
…………….
Na Ashrack Miraji Fullshangwe Media
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, leo amezindua rasmi Mradi wa Maji wa Same-Mwanga-Korogwe, akiwataka wananchi kuunganisha huduma ya maji, kulipa bili kwa wakati, na kutunza miundombinu ili kuhakikisha mradi huo unadumu kwa muda mrefu.
Akizungumza na wananchi wa mkoa wa Kilimanjaro katika viwanja vya CD Msuya, Rais Samia amesema serikali itaendelea kuwekeza katika miradi ya maji ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma safi na salama. Ameongeza kuwa maji ni nyenzo muhimu ya maendeleo, hivyo kila mmoja anapaswa kuwa sehemu ya ulinzi wa rasilimali hiyo.
Kwa upande wake, Waziri wa Maji Juma Aweso amempongeza Rais Samia kwa dhamira yake ya dhati ya kutatua changamoto za upatikanaji wa maji nchini. Ameeleza kuwa mradi huo umetekelezwa kwa ufanisi mkubwa, huku akiwashukuru watendaji na wasimamizi wa mradi kwa juhudi zao kuhakikisha mradi unakamilika kwa wakati na kwa viwango vilivyokusudiwa.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Nurdin Babu, amesema mradi huu utakuwa suluhisho la muda mrefu kwa wananchi wa maeneo husika ambao walikuwa wakikabiliwa na changamoto ya upatikanaji wa maji. Ameeleza kuwa maji haya yatachangia kuboresha maisha ya wananchi, kuinua uchumi wa mkoa, na kusaidia shughuli za kilimo na ufugaji.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akikagua moja ya sehemu ya kuchuja maji ya mradi wa Same-Mwanga-Korogwe mara baada ya hafla ya uzinduzi iliyofanyika Mwanga mkoani Kilimanjaro tarehe 09 Machi, 2025.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akiteta jambo na Waziri Mkuu Mstaafu Mzee Cleopa David Msuya mara baada ya kufungua mradi wa Maji wa Same-Mwanga-Korogwe kwenye hafla iliyofanyika Mwanga mkoani Kilimanjaro tarehe 09 Machi, 2025. Mzee Msuya pia aliwahi kuwa Mbunge wa Jimbo la Mwanga.
Taswira ya eneo la mtambo wa kutibu maji (Water treatment Plant ) katika mradi wa Maji wa Same-Mwanga-Korogwe uliopo wilayani Mwanga mkoani Kilimanjaro.