Kuwepo kwa vifaa maalumu katika mito nane ya Tanzania vitakavyoratibu na kubaini ujazo wa maji katika Bonde la Mto Nile itakuwa na manufaa kwa Serikali hasa katika ujenzi madaraja kwenye mito mbalimbali pamoja na kutoa taarifa za ujenzi wake kwa sekta husika.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji Mhandisi Mwajuma Waziri amesema hayo jijini Dodoma wakati wa zoezi la kusaini makubaliano ya uwekaji wa vifaa hivyo vya kuratibu hali ya ujazo wa maji ya mito hiyo inayotiririsha maji katika mto Nile.
“Lengo kubwa la vifaa hivi ni kuangalia mwenendo wa maji katika mito yetu, kupungua au kuongezeka ili kujua na kusaidia kutoa taarifa katika sekta mbalimbali za kimkakati kuhusu ujenzi wa miradi ya maendeleo kwenye mito yetu nchini,”.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Bonde la mto nile Dkt Florence Adongo amesema vifaa hivyo vitasaidia kulinda vyanzo vya maji na kuendelea kuwa na uoto wa asili kwenye mito hiyo zaidi ya arobaini katika idadi ya nchi kumi zinazopitiwa na mto Nile.