Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa Mheshimiwa Dkt. Stergomena Tax (Mb), tarehe 05 Machi, 2025, ameshiriki kikao cha Dharura cha Mawaziri wa Asasi ya Siasa, Ulinzi na Usalama ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) kilichofanyika kwa njia ya mtandao kujadili hali ya usalama katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.
Kikao hicho cha dharura cha Mawaziri kimejadili masuala ya amani Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) na jitihada mbalimbali ambazo Jumuiya ya SADC inaendelea kuchukua katika kutafuta amani ya kudumu Mashariki mwa DRC.
Kikao hicho cha Mawaziri wa SADC ni utangulizi wa kikao kitakachofanyika Tarehe 6 Machi, 2025, kitakachohusisha Wakuu wa Nchi na Serikali wa SADC wanaotarajiwa kukutana kwa njia ya Mtandao katika Mkutano wa Dharura wa Utatu wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Asasi ya Siasa, Ulinzi na Usalama (Extra-Ordinary Organ Troika Summit cha Nchi zinazochangia Vikundi vya Kijeshi katika Misheni ya Ulinzi wa Amani ya SADC nchini DRC (SAMIDRC) na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).