******************************************
Wanachama 883 wa Chadema wa kata ya Naberera Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara, wamehama chama hicho na kujiunga na CCM wakimfuata mbunge wa jimbo hilo James Ole Millya.
Wanachama hao walirudisha kadi zao jana kwenye kijiji cha Namaluli na kupokewa na katibu wa CCM wilayani Simanjiro Ally Kidunda.
Akizungumza baada ya wanachama hao kupokelewa Ole Millya alisema anawashukuru kwa kuamua kumfuata CCM kwani awali walikuwa wote Chadema.
Alisema yale mambo waliyokuwa wanalalamika awali hivi sasa hayafanyiki hivyo wamuunge mkono Rais John Magufuli ili wapatiwe maendeleo zaidi.
“Ninawashukuru mno kwa ninyi kuja CCM kama mimi kwa ajili ya kumuunga mkono Rais Magufuli mwenye maamuzi na moyo kama ya baba wa Taifa hayati mwalimu Julius Nyerere wa kusimamia maendeleo,”
Katibu wa CCM wa wilaya ya Simanjiro, Ally Kidunda aliwashukia vikali wanasiasa wanaoanza kujipitishapitisha kwa wanachama wa chama hicho kufanya kampeni kabla ya muda wa uchaguzi kufika.
Kidunda alisema watawachukulia hatua kali wanachama hao kupitia vikao vyao kwani yeye ndiye mtendaji wa chama hicho kwenye wilaya hiyo.
Alisema yeye ndiye mkurugenzi wa uchaguzi wa chama hicho hivyo hatakubali kuona viongozi wa CCM waliopo madarakani wanafanyiwa fitina na wanachama wa chama hicho kabla ya muda kufika.
Alisema mbunge wa jimbo hilo ni James Ole Millya hadi mwaka 2020 hivyo wanaohitaji kugombea nafasi hiyo wasubiri hadi kipindi hicho kwani wanaojipitisha hivi sasa watakuwa wanafanya makosa.
“Wanachama wa CCM mnapaswa kuanza kufanya fitina na kupitapita kwenye kata, vijiji au vitongoji vinavyoongozwa na viongozi wanaotokana na CCM,” alisema Kidunda.
Alisema hata nafasi za udiwani na wenyeviti wa vijiji na vitongoji wanaotokana na CCM wanapaswa kuachwa wamalize nafasi zao na siyo baadhi ya wanachama kuanza kampeni mapema.
Mmoja kati ya wanachama waliojiunga na CCM Raphael Mollel alisema ubabaishaji uliokuwa CCM awali ndiyo uliwakimbiza Chadema ndiyo sababu wamerejea CCM.
“CCM ya Simanjiro ilikuwa inakata majina ya watu na kuendeshwa kindugu tukahama ila sasa tumerudi kwenye chama chetu kumfuata mbunge wetu Millya ambaye tulikuwa naye Chadema,” alisema Mollel.