***************************
Asasi ya kiraia inayojihusisha na kuwasaidia watoto wa shule nchini, Tanzania Development Lightening Initiative (TDLI) imeanzisha kampeni ya kukusanya viatu jozi (pairs) 100 kwa ajili ya kusaidia wanafunzi wa shule za msingi wenye uhitaji.
Heri Ayubu, mwenyekiti wa TDLI amesema sio wanafunzi wote wanaoweza
kumudu sehemu ya gharama ya kununua sare za shule, vikiwemo viatu, hivyo katika utafiti wao walifanya kwa shule wanazozisaidia katika mikoa ya Mwanza na Dodoma, kuna uhitaji wa viatu jozi 100, ambazo zitavaliwa na wanafunzi 50, kwa wastani wa jozi mbili kwa mwanafunzi mmoja.
“Wanafunzi wanaotoka katika familia za kimaskini wana mahitaji mengi, tunadhani jamii ikitusaidia katika kampeni hii itaongeza chachu ya ufaulu wao,” amesema Ayubu.
Amesema tangu waanze kuzisaidia shule hizo miaka miwili iliyopita, ufaulu wa wanafunzi hao umeongezeka na wamekuwa wakijiona sehemu ya wanafunzi wengi.
“Mwanafunzi anaweza kukosa raha na hata wakati mwingine anaweza kushindwa mitihani yake kwa sababu anakwenda shule bila viatu au sketi yake imechanika, akijilinganishana wanafunzi wenzake anajiona tofauti,” anasema Ayubu.
Amesema nchi za Ulaya zina utaratibu wa kuwasaidia watu wasiojiweza, lakini kwa nchi nyingi za Kiafrika, jukumu hili bado linabaki katika jamii.
Amesema kuna haja ya jamii ya Kitanzania kujenga utamaduni wa kuwasaidia watoto wenye uhitaji na kuchangia mahitaji yao, kama wanavyochangia katika sherehe za harusi, misiba na siku za kuzaliwa.
Pia amesema kuna baadhi ya mashirika na watu binafsi wenye utamaduni wa kujumuika na kula pamoja na watoto wenye uhitaji likiwa ni jambo zuri, lakini TDLI inadhani kula nao pekee haitoshi, bali msaada ya kimkakati yenye lengo la kuwajengea misingi watoto maskini kukabiliana na maisha na kuwa chachu ya maendeleo ya Taifa, akitolea mfano misaada inayokusidia kuwapa Elimu bora na huduma za Afya.
Mshauri wa TDLI, Lilian Simule amesema wanachama wa asasi yao wamekuwa na utamaduni wa kuchangia fedha au vifaa wakati wanaadhimisha siku zao za kuzaliwa.
Akiadhimisha sherehe za kuzaliwa kwake, Simule aliendesha harambee yakuchangia sehemu ya hitaji la viatu v, ambapo waalikwa walichangia pesa taslimu na wengine kuweka ahadi, pesa zote vikifikia zaidi ya 450,000.
“Kiasi hiki kidogo tulichopata kitatuwezesha kupata walau jozi 30 kwa kuanzia, hivyo tunaomba wengine watusaidie, kwa kutoa pesa au kutuletea viatu na vitu vingine kwa ajili ya mahitaji yao ya shule,” amesema.
“Watoto hawahitaji mahitaji makubwa na mengi yapo ndani ya uwezo wetu tukiamua kutoa kile kidogo tunachokipata;”
“Sisi, TDLI sio matajiri, bali tuna moyo, hivyo ikiwa watu watachangia japo shilingi elfu kumi kila mmoja au kiasi chochote tutafanikiwa kuwasaidia watoto kutoka kaya maskini wenye mahitaji ya kielimu ili baadae wawe na ushindani katika soko la ajira,”amesema Simule.
“Lakini hata mtu akichangia kalamu, vitabu na madaftari pia tutapokea misaada hiyo,” amesema Simule.
Asasi ya TDLI inaendesha shughuli zake kwa kutumia michango ya wanachama wake na wadau mbalimbali pamoja na shughuli za kuingiza kipato kwa ajili ya kazi zake, hivyo kupunguza utegemezi wa ufadhili wa wahisani pekee tofauti na Asasi nyingine nyingi hapa nchini.
Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa TDLI, Asasi ya TDLI inawakutanisha vijana kutoka katika kada mbalimbali ili kuunganisha nguvu zao katika kurudisha fadhila kwa jamii ya Tanzania wakiunganishwa na Imani kuwa maendeleo endelevu yatapatikana endapo wanajamii watachangia kuondoa tofauti ya mahitaji ya msingi kama vile Elimu bora na huduma za afya kwa wanajamii walio na changamoto za kiuchumi.
Ayubu amesema wale watakaoguswa wanaweza kutuma walichojaaliwa kupitia MPESA namba 0744333344 kwa jina la Tanzania Devt Lightening Initiative. Ameongeza kuwa TDLI wanao utaratibu wa kuhakikisha mrejesho unatolewa kwa mchangiaji kuhusu utekelezwaji wa malengo
yaliyokusudiwa.