Meneja wa TANROADS Mkoa wa Ruvuma Saleh Juma aliyeshika magoti,akiangalia vipimo vinavyoonesha ubora wa lami iliyowekwa kwenye wa barabara ya Amanimakolo-Ruanda Wilaya ya Mbinga hadi Bandari ya Ndumbi Wilaya ya Nyasa Mkoani Ruvuma.
Ujenzi wa Barabara la lami ya Amanimakolo-Ruanda Wilaya ya Mbinga hadi Bandari ya Ndumbi Wilaya ya Nyasa Mkoani Ruvuma ukiendelea kama inavyoonekana.
Muonekano wa sehemu ya barabara ya lami ya Amanimakolo-Ruanda Wilaya ya Nyasa kuelekea Bandari ya Ndumbi Wilaya ya Nyasa Mkoani Ruvuma ikiwa ni sehemu ya Mafanikio ya miaka minne ya Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Dkt Samia Suluhu Hassan.
Meneja mradi wa Ujenzi wa Barabara ya lami ya Amanimakolo-Ruanda Wilaya ya Mbinga hadi Bandari ya Ndumbi Wilaya ya Nyasa Mkoa wa Ruvuma kutoka Kampuni ya China Railway Seventh Group(CRSG) GE Guanghua wa pili kushoto,akitoa taarifa ya maendeleo ya mradi huo kwa Meneja wa Wakala wa Barabara Tanzania(TANROADS) Mkoa wa Ruvuma Saleh Juma wa tatu kushoto.
………
Na Mwandishi Maalum, Mbinga
WAKALA wa Barabara Tanzania(TANROADS)Mkoa wa Ruvuma,umeanza ujenzi wa awamu ya pili ya sehemu ya barabara ya Amanimakolo-Ruanda hadi Bandari ya Ndumbi yenye urefu wa kilometa 95 kwa kiwango cha lami.
Meneja wa TANROADS Mkaoni Ruvuma Saleh Juma amesema,ujenzi wa barabara hiyo unafanyika kwa awamu tatu,awamu ya kwanza imehusisha kipande cha barabara kutoka Kitai hadi kijiji cha Amanimakolo chenye urefu wa kilometa 5 ambayo imekamilika na kuanza kutumika.
Alisema,sehemu ya pili ya ujenzi imeanza kijiji cha Amanimakolo hadi kijiji cha Ruanda Wilaya ya Mbinga urefu wa kilometa 35 ambapo Mkandarasi anakamilisha kuweka tabaka la lami kipande cha kilometa 2 kati ya 35.
Aidha alisema,ujenzi wa barabara hiyo ni sehemu ya mafanikio ya miaka minne ya Serikali ya awamu ya sita ya Rais Samia Suluhu Hassan na awamu ya tatu itaanza katika kijiji cha Ruanda Wilaya ya Mbinga hadi Bandari ya Ndumbi Wilayani Nyasa
“ujenzi wa Bandari ya Ndumbi umekamilika miaka miwili iliyopita,kinachosubiriwa ni kukamilika kwa barabara ili bandari ianze kutumika kusafirisha bidhaa kutoka Mkoa wa Ruvuma kwenda mikoa mingine na nchi jirani ya Malawi”alisema Saleh.
“Sisi TANROADS tumeanza kutekeleza mradi huu na hatujakwama,Serikali inaendelea kutupatia fedha kwa ajili ya kukamilisha kazi japokuwa tumechelewa ili kumaliza adha ya vumbi kwa Wananchi linalotokana na magari yanayobeba makaa ya mawe kutoka mgodini kuja Bandari kavu kijiji cha Amanimakolo.”alisema Saleh.
Alisema,baada ya kukamilisha awamu ya pili wataendelea na ujenzi wa awamu ya tatu kutoka kijiji cha Ruanda kuelekea Lituhi hadi Bandari ya Ndumbi ambapo Wananchi wa maeneo hayo wana uhitaji mkubwa wa miundombinu bora ya barabara ili waweze kusafirisha bidhaa hasa samaki na dagaa wanaopatikana kwa wingi katika Ziwa Nyasa nyingine.
Alisema,wataweka lami sehemu zote korofi ili kutatua kero ya usafiri kwa Wananchi ili waweze kufurahia matunda ya serikali yao ya awamu ya sita ambayo imejipanga kumaliza kero mbalimbali za kijamii ikiwemo ubovu wa miundombinu ya barabara.
Kwa upande wake Mhandisi kutoka Ofisi ya Meneja wa TANROADS Mkoa wa Ruvuma Anselem Chambila alisema,katika mradi huo kati ya kilometa 35 zilizopo kwenye mpango wa awamu ya pili wameanza ujenzi wa kilometa tano kati ya hizo kilometa mbili ziko hatua ya mwisho kukamilika.
Alisema,utekelezaji wa mradi huo unaendelea vizuri na wanachosubiri ni kupata fedha kutoka Serikalini kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa kilometa zote 35 ili Wananchi waweze kutumia barabara hiyo kwa kusafiri na kusafirisha bidhaa zao.
Naye Meneja mradi wa Kampuni ya China Railway Seventh Group(CRSG) inayojenga barabara hiyo GE Guanghua alisema,hadi sasa wamefikia asilimia 40 ya utekelezaji wake.
Baadhi ya Wananchi wa kijiji cha Amanimakolo,wameipongeza Serikali kwa kuendelea na ujenzi wa barabara ya lami, kwani itakapokamilika itasaidia kurahisisha shughuli za usafiri na kuharakisha maendeleo yao.
Hata hivyo, wameimtaka TANROADS kumsimamia kwa karibu mkandarasi ili aweze kukamilisha ujenzi wa barabara hiyo haraka kwa kuwa ujenzi wake umechukua muda mrefu bila kukamilika.