*Awasilisha mpango wa Mining Vision 2030
*Serikali yajipanga kuongeza eneo kubwa zaidi lililofanyiea Utafiti wa Madini wa kina
*Kampuni za Utafiti Madini zakaribishwa Tanzania
*Aelekeza STAMICO kufanikisha upatikanaji wa vifaa ya Utafiti wa awali kwa ajili ya wachimbaji wadogo
𝐓𝐨𝐫𝐨𝐧𝐭𝐨,𝐂𝐚𝐧𝐚𝐝𝐚
Waziri wa Madini Mh. Anthony Mavunde amezikaribisha nchini Tanzania Kampuni za Utafiti wa madini kushirikiana na serikali katika kutimiza malengo ya Mining VISION2030 ambayo imejikita katika kufanya utafiti wa kina wa madini kufikia eneo la ukubwa wa asilimia 50 kufikia mwaka 2030.
Mh. Mavunde ameyasema hayo jana Toronto,Canada wakati akihutubia kikao cha Mawaziri wa Madini kutoka nchi mbalimbali duniani,Kampuni za Utafiti na Uendelezaji Migodi na Asasi za kiraia.
“Serikali ya Tanzania chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia S. Hassan imeweka mazingira wezeshi ya kiuwekezaji,hivyo ni fursa kubwa ya Kampuni za Utafiti kuja kushirikiana na Serikali ya Tanzania katika mkakati wake wa kuongeza eneo lililofanyiwa utafiti wa kina wa madini.
Kwa sasa Serikali kupitia Wizara ya Madini,inatekeleza mpango wa utafiti wa madini wa kina kutoka eneo la utafiti wa kina la asilimia 16 kufikia eneo la asilimia 50 kufikia mwaka 2030.
Kwa kuwa Tanzania ni kisiwa cha amani,uongozi imara na mazingira mazuri ya kiuwekezaji nichukue fursa hii kuwakaribisha wadau kuungana na serikali katika mpango wake huu wa utafiti wa kina wa madini nchini kwa kuwa serikali peke yake haiwezi kufanya kwa eneo lote hivyo sekta binafsi ni muhimu katika kufikia azma“Alisema Mavunde
Awali akiwa katika mabanda ya maonesho ya vifaa vya Madini,akiongozana na Balozi wa Tanzania nchini Canada Mh. Joseph Sokoine na wataalamu wa Wizara ya Madini,Waziri Mavunde amemuelekeza Mkurugenzi Mtendaji wa STAMICO Dkt. Venance Mwasse kuangalia namna ya upatikanaji wa vifaa vya utafiti wa awali wa madini ili wakati wachimbaji wadogo wakipata huduma ya uchorongaji kuwepo pia vifaa vya awali vya kusaidia kuonesha maeneo yanayopaswa kuchorongwa.