Na Ali Issa Malezo 4/3/2025.
Wizara ya Utalii na mambo ya Kale Zanzibar imewapatia mafunzo maalum watembeza watalii 150 (Beach Boys) ili kuona kazi hiyo inafanywa vizuri kwa kulinda maslahi ya Zanziabr na tamaduni zisipotee.
Yamesemwa hayo leo huko Maruhubi katika Chuo cha Hoteli na Utalii na Mkurugenzi wa Utalii Dkt. Abdallah Mohamed wakati alipokuwa akizundua mafunzo hayo ya siku tatu kwa vijana wanao tembeza watalii hapa Zanzibar.
Amesema utalii ni sekta muhimu Zanzibar ambayo unaongeza pato la Taifa na wananchi wengi kufaidika na sekta hiyo, hivyo kupatiwa vijana mafunzo hayo ni wajibu kwani kutapelekea mustakabali mzuri kwa watembaza watalii pamoja na kuilinda hazina hiyo isipotoshwe na kuharibiwa.
“Tunalinda hazina ya utalii zanzibar hatuwezi kuwaacha kufanya kazi kiholela usiharibiwe utalii isiharibiwe na tumebaini wapo baadhi ya watembeza watalii hawana taluma ya kutosha katika masuala ya tuor gaide,lakini wapo hawapo leseni (vitambulisho) wanafanya kazi kwa mazoea, hivyo mafunzo haya matarajio yetu kuona vijana hawa wanafanya kazi kwa ustadi mkubwa kuwahudumia watali”alisema Mkurugenzi huyo.
Aidha alisema kuwa mafunzo hayo pia yatafanyika Pemba kwani Kisiwa hicho kinafunguka kiutalii.
Naye Mkufunzi wa mafunzo hayo Ali Hassan Ali Afisa kutoka Wizara ya Utalii na mambo ya kale alisema kuwa taaluma wanayoitoa kwa vijana hao ni kuwajengea uwezo pamoja na kuifahamu Zanzibar na mazingira yake ikiwemo historia ya nchi, utamaduni wa watu wake na hali halisi ya watu wa Zanzibar walivyo bila ya kupoteza ukweli.
Aidha alisema kuwa Wizara imebaini wapo baadhi ya watembeza watalii hawana taaluma ya kutembeza watalii hivyo wakaona ipo haja ya kuwapatia mafunzo hayo.
Nae mmoja wa washiriki wa mafunzo hayo Ali Omari Masoud amesema anashukuru kupata mafunzo hayo kwani yatawapa weledi wa kujua yale ambayo aliyokuwa hayajui na yatamjengea uwezo katika kazi zake.
Mafunzo hayo ya siku tatu yamejumuisha watembeza watalii 150 ambapo mada mbalimbali zimeandaliwa ikiwemo kuzijuwa sehemu za hitoria ya Zanzibar, fukwe safi, hoteli kubwa, sehemu wanazo zipenda wageni na wanachohitaji wageni katika maeneo wanayo yatembelea.