*Lengo ni kuvutia wawekezaji wengi zaidi Sekta ya Mafuta
*Tanzania kuongeza kasi ya utafutaji wa mafuta.
*Vituo zaidi ya vitano vya CNG kujengwa kwenye mikoa ambayo haijafikiwa na Bomba la Gesi
Kamishna wa Petroli Wizara ya Nishati, Goodluck Shirima amesema Tanzania imejipanga vema kama nchi mwenyeji wa Mkutano na Maonesho ya 11 ya Petroli Afrika Mashariki kwa kuhakikisha sekta binafsi inashirikishwa kikamilifu kwenye uwekezaji wa miradi ya mafuta na gesi.
Shirima ameyasema hayo leo 26 Februari, 2025 katika Kipindi cha Goodmorning cha Wasafi FM kilichohusu ujio wa Mkutano wa 11 wa Petroli utakaofanyika tarehe 5 hadi 7 Machi, 2025 katika ukumbi wa JNICC jijini Dar es Salaam, ikiwa ni muendelezo wa kuhamasisha umma juu ya ujii wa mkutano huo.
Amesema kupitia EAPCE’25 fursa mbalimbali za uwekezaji zitatangazwa pamoja na kunadi duru ya tano ya vitalu vya mafuta na gesi asilia kwa ajili ya maeneo ya uwekezaji yapatayo 26 ambapo amewataka wawekezaji kutoka pande zote za Afrika Mashariki, kampuni kubwa za mafuta na gesi kutoka nje ya nchi na ndani ya nchi kutumia vema fursa hiyo.
‘’Tunawakaribisha sana wawekezaji kuja kuwekeza kwenye sekta ya mafuta kwa kuwa tutabadilishana uzoefu na wenzetu ambao wameshagundua mafuta na gesi na kujifunza kutoka kwao hususani kwa nchi za Uganda na Kenya.” Amesema Shirima
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Mipango na Uwekezaji kutoka Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) Derrick Moshi amesema, katika kuchagiza sekta ya mafuta na gesi tayari TPDC inatekeleza miradi mbaimbali ya gesi ikiwemo kufunga miundombinu ya gesi kwenye maeneo yanayopitiwa na bomba la gesi, vituo vya kujaza gesi kwenye magari pamoja na kukamilisha kituo mama cha kujaza gesi kwenye magari kwa Mkoa wa Dar es Salaam eneo la Chuo Kikuu jijini Dar es Salaam.
Amesema kwa mwaka huu TPDC inatarajia kuzindua vituo 6 vya CNG ambapo mwezi ujao kitazinduliwa kituo kikubwa cha CNG katika eneo la Ubungo jijini Dar es Salaam.